Jeshi la Sudan lafanya mashambulizi ili kudhibiti mji wa Khartoum
Jeshi la Sudan leo Alhamisi limefanya mashambulizi ya anga na ya mizinga katika mji mkuu wa Sudan, Khartoum katika operesheni iliyotajwa kuwa kubwa zaidi ya kudhibiti mji huo mkuu tangu kuanza vita kati yake na Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) miezi 17 iliyopita.
Mashambulizi ya leo ya jeshi la Sudan ambalo lilipoteza udhibiti wa mji mkuu Khartoum mwanzoni mwa vita kati yake na RSF, yamefanyika kabla ya hotuba ya kamanda wa jeshi hilo, Jenerali Abdel Fattah al Burhan, katika Mkutano wa 79 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York.
Mashuhuda wamesema kuwa, sauti kubwa za mashambulizi na mapigano zimesikika leo wakati vikosi vya jeshi la Sudan vilipojaribu kuvuka madaraja ya juu ya Mto Nile yanayounganisha miji mitatu ya Sudan yanayounda mji mkuu.
Wakati huo huo ripoti zinasema kuwa wapiganaji wa kikosi cha RSF pia wameendelea kusonga mbele katika maeneo mengine ya Sudan katika miezi ya karibuni katika mzozo ambao umesababisha maafa makubwa ya binadamu huko Sudan.
Hadi sasa watu zaidi ya watu milioni kumi wamelazimika kuhama makazi yao na baadhi ya maeneo ya Sudan yamekumbwa na njaa kufuatia vita baina ya pande mbili.