Pasta aliyebaka na kuua nchini Kenya akutwa na hatia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i11704-pasta_aliyebaka_na_kuua_nchini_kenya_akutwa_na_hatia
Pasta wa kanisa moja la kipendekosti nchini Kenya anasubiria hukumu ya kifo dhidi yake baada ya mahakama ya nchi hiyo hapo jana Alkhamis kumkuta na hatia ya kumuua muumini wake baada ya kumbaka.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 21, 2016 23:33 UTC
  • Pasta aliyebaka na kuua nchini Kenya akutwa na hatia

Pasta wa kanisa moja la kipendekosti nchini Kenya anasubiria hukumu ya kifo dhidi yake baada ya mahakama ya nchi hiyo hapo jana Alkhamis kumkuta na hatia ya kumuua muumini wake baada ya kumbaka.

Kwa mujibu wa taarifa, Paul Ng’ang’a wa dhehebu la Wells of Faith lililoko mtaa wa Dagoreti alifanya jinai hiyo ya kubaka na kumuua Bi, Caroline Chinjira hapo tarehe 17 mwezi Machi, 2012. Baada ya mahakama kumkuta na hatia pasta huyo, Jaji Jessie Lessit iliamuru kurejeshwa jela hadi tarehe 25 ya mwezi huu atakaposomewa hukumu dhidi yake ambayo kwa mujibu wa sharia za nchi hiyo ni adhabu ya kifo.

Ni Pasta Paul Ng’ang’a akiwa mahakamani

Aidha mahakama ilifutilia mbali dhamana aliyokuwa amepewa Pasta huyo muuaji. Inaelezwa kuwa, waumini wa kanisa la Pasta Paul Ng’ang’a, walikasirishwa mno na kitendo hicho cha mhubiri huyo, ambapo walifanya msako mkali wa kumtafuta baada ya kujiri tukio la mauaji miaka mine iliyopita. Baada ya kumtia mbaroni waumini hao walimpeleka moja kwa moja polisi na kufunguliwa mashtaka ya mauaji.

Pasta Paul Ng’ang’a

Kadhalika Jaji Lessit jana alimwachilia huru Paul Muia aliyekuwa akishtakiwa pamoja na Pasta Ng’ang’a katika faili hilo, baada ya kumkosa na hatia. Jaji alisema Bi, Caroline Chinjira ambaye alikuwa muumini wa kanisa alilohudumu Pasta Ng’ang’a alifariki dunia kutokana na jeraha la kuchomwa kisu kifuani. Kabla ya kuuawa mwanamke huyo alibakwa ambapo imearifiwa kuwa alijitahidi kujiokoa bila mafanikio. Mashahidi waliofika mahakamani walimtaja pasta huyo kuwa muhusika mkuu wa jinai huku uchunguzi wa DNA uliofanyiwa chembe chembe zilizotolewa kutoka kwa Pasta Ng’ang’a zikiambatana na shahawa zilizokutwa katika sehemu za siri za marehemu.