Rwanda yazindua kampeni ya chanjo ya Marburg
(last modified Mon, 07 Oct 2024 02:20:01 GMT )
Oct 07, 2024 02:20 UTC
  • Rwanda yazindua kampeni ya chanjo ya Marburg

Rwanda imeanza kutoa dozi za chanjo ya virusi vya Marburg ili kujaribu kudhibiti mripuko wa ugonjwa huo unaofanana na Ebola katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki.

Sambamba na kutangaza kuanza kwa kampeni hiyo ya chanjo jana Jumapili, Waziri wa Afya wa Rwanda, Sabin Nsanzimana amesema katika kikao na wanahabari kuwa, "Kampeni ya chanjo itazingatia zaidi wale walio hatarini zaidi, wafanyakazi wa afya wanaohudumu katika vituo vya matibabu, hospitalini, katika vyumba vya wagonjwa mahututi ICU, katika dharura, lakini pia wenye mawasiliano ya karibu na kesi zilizothibitishwa."

Waziri Nsanzimana ameeleza bayana kuwa, serikali ya Kigali inaamini kuwa, kupiga chanjo ni muhimu sana katika kuzuia kuenea kwa virusi hivyo hatari. Hii ni mara ya kwanza kwa Marburg kuthibitishwa nchini Rwanda.

Rwanda imethibitisha vifo 12 na kesi 46 za ugonjwa wa Marburg tangu kuripotiwa mripuko huo mnamo Septemba 27. Watu 29 walioambukizwa maradhi hayo hatarishi ya kuambukiza wamewekwa karantini.

Ugonjwa wa Marburg husababishwa na virusi vinavyoshabihiana na Ebola na hata dalili zake hazina tofauti kubwa na ugonjwa wa Ebola.

Dalili za ugonjwa huo ni pamoja na kikohozi, maumivu ya viungo, kuharisha na kutapika, na mara nyingi hata upungufu wa damu mwilini.