Misri yakanusha tuhuma za Hemedti kuwa inahusika katika mashambulizi ya anga dhidi ya RSF
-
Mohamed Hamdan Dagalo
Misri mekanusha tuhuma zilizotolewa na kamanda wa Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF) nchini Sudan, Mohamed Hamdan Dagalo (Hemedti), kwamba nchi hiyo inashiriki katika mashambulizi ya anga dhidi ya vikosi vyake katika eneo la Jabal Muya katika jimbo la Sennar, katikati mwa Sudan.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Misri imesema katika taarifa yake iliyochapishwa kwenye mitandao ya kijamii usiku wa kuamkia leo, kwamba jeshi la Misri halishiriki katika vita vinavyoendelea nchini Sudan, na kuitaka jamii ya kimataifa kuomba ushahidi wa kuthibitisha madai yaliyotolewa na Jenerali Hamdan Dagalo.
Hemedti ameituhumu Misri kuwa inashiriki katika mashambulizi ya anga dhidi ya vikosi vya RSF katika eneo la Jabal Muya, na kusema kwamba majeshi yake "yameuawa na kushambuliwa kwa hila na ndege za kivita za Misri."
Hemedti pia ameituhumu Cairo kuwa inatoa mafunzo kwa jeshi la Sudan na kulipatia ndege zisizo na rubani huku vita vikiendelea nchini Sudan kati ya jeshi la serikali na waasi wa Rapid Support Forces.
Jumamosi iliyopita, jeshi la Sudan lilitangaza kuwa limekomboa eneo la Jabal Muya katika Jimbo la Sennar, baada ya mapigano makali yaliyoendelea kwa siku kadhaa.