Rais William Ruto ameiomba Mahakama ya Milimani kutupilia mbali kesi za Gachagua
Rais William Ruto wa Kenya ameiomba Mahakama Kuu kutupilia mbali kesi kadhaa za kupinga kuondolewa madarakani Rigathi Gachagua kama Naibu Rais, akisema kuwa masuala yaliyoibuliwa katika kesi hizo yametengewa Mahakama ya Juu pekee.
Dr. Ruto amesema katika majibu yake kwamba kesi zilizowasilishwa zinakiuka Kifungu 140 kama kinavyosomwa pamoja na vifungu vya 148 na 149 vya Katiba, ambavyo vinaitwika Mahakama ya Juu, mamlaka ya kuamua mizozo inayotokana na mchakato wa uchaguzi wa urais.
Bw. Gachagua na wenzake waliwasilisha mashtaka mahakamani wakipinga mchakato wa kuondolewa kwake madarakani kwa tuhuma kadhaa.
Gachagua alitimuliwa na Bunge la Seneti la Kenya Alkhamisi iliyopita kwa mashtaka matano kati ya 11 yaliyowasilisihwa dhidi yake, yakiwemo kuchochea migawanyiko ya kikabila na kuhujumu Idara ya Mahakama.
Hata hivyo aliwasilisha rufaa mahakamani akisema uamuzi wa kumuondoa madarakani haukufanyika kwa mujibu wa sheria.
Naibu huyo wa Rais wa Kenya aliyetimuliwa, leo Jumanne amehudhuria kikao cha Mahakama Kuu inayosikiliza kesi mbili za kupinga kuondolewa kwake mamlakani.
Bw. Gachagua alifika katika Mahakama ya Milimani jijini Nairobi akiwa na msafara wa magari sita akiandamana na Mbunge wa Embakasi ya Kati, Benjamin Gathiru, maarufu kama Major Donk, aliyekuwa Katibu Mkuu wa United Democratic Alliance (UDA) Cleophas Malala na mawakili kadhaa.
Jopo la majaji watatu katika Mahakama Kuu jijini Nairobi limeanza kusikiliza rufaa ya Gachagua.