Raia 46 wauawa katika mapigano mapya nchini Sudan
Takriban raia 46 wameuawa huku wengine 44 wajeruhiwa katika siku mbili za mapigano kati ya jeshi la Sudan na Kikosi cha Radimali ya Haraka (RSF) katika majimbo ya Khartoum na Al-Jazira.
Wizara ya Afya na mashirika ya kujitolea yalisema hayo Jumanne na kuongeza kuwa, msichana mmoja aliuawa na watu wengine 17 walijeruhiwa, wakiwemo watoto wanane, kutokana na mashambulizi ya mizinga katika mji wa Omdurman, nje kidogo ya Khartoum.
Wizara hiyo imewashutumu vikali wapiganaji wa RSF kwa kutekeleza shambulizi hilo lililoathiri vitongoji katika maeneo ya Al-Thawra na Al-Fath.
Katika hatua nyingine, Idara ya Dharura ya eneo la Ukanda wa Kusini wa Khartoum imesema kuwa, raia 20 waliuawa na wengine 27 kujeruhiwa jana Jumanne kutokana na shambulio la anga kwenye kitongoji cha Mayo kusini mwa Khartoum.
Katika jimbo la mashariki la Al-Jazirah, Kamati ya Upinzani ya Jiji la Rufaa, kikundi cha kujitolea kusaidia wahasiriwa wa vita, ilitangaza kuwa raia 25 waliuawa huku kadhaa wakijeruhiwa katika mashambulizi ya RSF.
Mapigano ya silaha yalianza huko Sudan Aprili 15 mwaka jana kati ya jeshi la nchi hiyo (SAF) linaloongozwa na Jenerali Abdel Fattah al Burhan ambaye ni kiongozi wa Sudan na wanamgambo wa RSF ambao kamanda wao ni Hamdan Dagalo. Hadi sasa juhudi za upatanishi wa kimataifa za kuhitimisha mapigano hayo yaliyoua maelfu ya watu na kulazimisha mamilioni kuwa wakimbizi ndani na nje ya nchi zimegonga mwamba.