Vikosi vya usalama Tunisia vyawatia mbaroni wafanya magendo 205 wa mihadarati
(last modified Fri, 25 Oct 2024 10:12:33 GMT )
Oct 25, 2024 10:12 UTC
  • Vikosi vya usalama Tunisia vyawatia mbaroni wafanya magendo 205 wa mihadarati

Wizara ya Mambo ya Ndani ya Tunisia imetangaza katika taarifa yake ya jana kwamba, vikosi vya usalama vya nchi hiyo vimefanikiwa kusambaratisha mtandao mkubwa wa magendo ya dawa za kulevya na kuwakamata watu 205 wanaohusika na magendo hayo.

Taarifa ya wizara hiyo imesema: "Kufuatia maagizo ya Rais wa Tunisia Kais Saied la kuongeza juhudi maradufu za kusambaratisha mitandao ya wahalifu, hasa wanaojihusisha na magendo ya dawa za kulevya, vikosi vya usalama wa taifa vimeanzisha operesheni kubwa na ya wakati mmoja ya usalama jana alfajiri Oktoba 24, 2024, ikiwalenga wafanyabiashara wa dawa za kulevya na wahalifu hatari."

Mbali na kuwatia mbaroni wafanya magendo hao wa mihadarati katika eneo la Grand Tunis, ambalo ndilo eneo kubwa zaidi la la makazi ya watu nchini Tunisia ambalo linajumuisha magavana wa Tunis, Ariana, Manouba na Ben Arous, vikosi vya usalama vya nchi hiyo vimefanikiwa pia kukamata kiasi tofauti cha dawa za kulevya, fedha na silaha za mapanga.

Jeshi la Polisi nchini Tunisia

 

Sehemu moja ya taarifa ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Tunisia imesema: "Chini ya usimamizi wa maafisa wakuu wa usalama na kwa uratibu na ofisi ya mwendesha mashtaka wa umma, vikosi vya usalama na walinzi wa Taifa vimeendesha msururu wa operesheni zinazowalenga wasafirishaji haramu (wa mihadarati) na wahalifu hatari zaidi.

Taarifa hiyo pia imesema: "Watu 205 hatari wamekamatwa. Operesheni hiyo pia imepelekea kukamatwa kiasi mbalimbali cha dawa za kulevya, silaha za mapanga na kiasi fulani cha fedha. Hatua hii iliyoratibiwa kwa uangalifu mkubwa inaonesha azma ya Serikali ya kusambaratisha mitandao hii ya uhalifu inayoathiri eneo letu lote."