Mapigano kati ya majenerali wa kijeshi yazidi kuinakamisha Sudan
(last modified Fri, 25 Oct 2024 10:13:18 GMT )
Oct 25, 2024 10:13 UTC
  • Mapigano kati ya majenerali wa kijeshi yazidi kuinakamisha Sudan

Mapigano ya uchu wa madaraka baina ya majenerali wa kijeshi wanaoongoza makundi mawili ya SAF na RSF yameongezeka katika maeneo mengi ya Sudan na kusababisha hasara kubwa kwa raia.

Duru mbalimbali za kieneo zimetangaza kuwa, katikati mwa Sudan, Jeshi la nchi hiyo SAF linaloongozwa na Jeneral Abdul Fattah al Burhan lilirejesha udhibiti wake wa mji wa Al-Suki wa jimbo la Sinnar jana Alkhamisi. Mji huo ulikuwa unadhibitiwa na Vikosi vya Msaada wa Haraka vinavyoongozwa na jenerali mwingine wa kijeshi, Mohamed Hamdan Dagalo maarufu kwa jina la Hemedti. 

Muungano wa Vijana wa Sinnar ambacho ni kikundi cha kujitolea cha jimbo hilo nacho kimedhitisha taarifa ya kutekwa tena mji wa Al-Suki na jeshi la Sudan. Mji huo ulikuwa umetekwa na kundi la RSF tarehe 25 Julai mwaka huu. 

Wahahnga wakuu wa vita vya uchu wa madaraka baina ya wanajeshi wa Sudan, ni raia wa kawaida

 

Tab'an maana ya kubadilishana udhibiti baina ya makundi hayo mawili ya wanajeshi hakuna matokeo mengine isipokuwa kuzidi kuunakamisha mji huo na maeneo mengine ya Sudan kutokana na silaha nzito za kijeshi zinazotumika kushambulia maeneo ya pande hasimu. 

Wakati huo huo, mtandao usio wa kiserikali wa madaktari wa Sudan umetoa taarifa na kusema kuwa, watu 11 wameuawa na wengine wengi kujeruhiwa katika shambulio la kundi la RSF kwenye kijiji cha Maknoon cha mashariki mwa Jimbo la Gezira la katikati mwa Sudan.

Karibu na mji mkuu Khartoum pia, mtu mmoja amenukuliwa akisema kuwa, ameshuhudia mapigano makali yakitokea jana asubuhi katika vitongoji vya Jabra na Mayo vya kusini mwa Khartoum.

Zaidi ya watu 24,850 wameshauawa nchini Sudan tangu vilipozuka vita baina ya makundi mawili ya wanajeshi mwezi Aprili 2023.