Ripoti ya UN yaonya kuhusu njaa kali Congo DRC, migogoro inaendelea
(last modified Wed, 30 Oct 2024 09:24:33 GMT )
Oct 30, 2024 09:24 UTC
  • Ripoti ya UN yaonya kuhusu njaa kali Congo DRC, migogoro inaendelea

Ripoti ya hivi karibuni ya Umoja wa Mataifa inaeleza kwamba karibu mtu mmoja kati ya wanne katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) anasumbuliwa na njaa kali, huku mamilioni ya watu wakilazimika kuyahama makazi yao.

Ukosefu huo mkubwa wa usalama wa chakula unaathiri takriban watu milioni 25.6 ambao maisha na riziki zao ziko katika "hatari ya muda mfupi kutokana na ukosefu wa chakula."

Ripoti hiyo inaashiria sababu mbalimbali zinazochangia uhaba huo mkubwa wa chakula, ikiwa ni pamoja na migogoro inayoendelea kwa sasa katika nchi hiyo ya Kiafrika, kupanda kwa bei za vyakula, na kupanda kwa gharama za usafiri, sambamba na athari za muda mrefu za magonjwa kadhaa ya mlipuko, kama vile surua, kipindupindu, malaria na mpox.

Mgogoro wa njaa unaathiri nchi nzima ya Congo DR, ikiwa ni pamoja na mji mkuu, Kinshasa, ingawa mikoa iliyoathiriwa na migogoro inaripoti takwimu za kutisha zaidi. Mikoa kama Kivu Kaskazini, Ituri na Kivu Kusini, ambayo imesumbuliwa na migogoro ya muda mrefu ya binadamu, imeonekana kuzorota zaidi kutokana na mzozo mpya wa waasi wa M23.

Congo DR

Kuhama makazi kwa idadi kubwa ya watu kumeongeza mgogoro huo, huku Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) likiripoti kuwa, katika maeneo hayo, asilimia 25 ya wamiliki wa mifugo wamepoteza mifugo yao, na 35% ya kaya zimeshindwa kulima.