Wafuasi wa kundi lenye misimamo mikali waua, kujeruhi 16 Uganda
Watu kadhaa wanaoshukiwa kuwa wafuasi madhehebu ya kidini yenye misimamo ya kufurutu ada wameshambulia kijiji kimoja nchini Uganda, na kuua watu wasiopungua wanane, akiwemo mtoto wa umri wa miaka mitatu na watu wa familia za washambuliaji hao.
Vyombo vya usalama vimeripoti habari hiyo leo Jumatano na kueleza kuwa, shambulio hilo lilitokea Jumanne usiku huko Muzizi A, kijiji kidogo kilichoko katika wilaya ya Kagadi magharibi mwa Uganda, yapata kilomita 250 kutoka mji mkuu Kampala.
Gazeti la Daily Monitor limeandika habari hiyo na kunukuu maafisa usalama wakieleza kuwa, watu wengine wanane walijeruhiwa katika shambulio hilo.
"Taarifa za awali zinaonyesha kuwa, wafuasi wa madhehebu hiyo mpya ambayo haijajulikana waliwashambulia wanakijiji ambao wengi wao ni watu wa familia zao, na kuwakatakata," Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Uganda UPDF limesema.
Maafisa usalama kutoka jeshi na polisi wameanzisha operesheni ya kuwasaka wahalifu huku uchunguzi ukiendelea ili kupata maelezo zaidi kuhusu tukio hilo. Wanne kati ya waliouawa walikuwa na umri wa chini ya miaka 13, akiwemo mtoto wa miaka mitatu, polisi walisema.
Polisi walisema washukiwa wawili wa waliotekeleza unyama huo wameuawa na vikosi vya usalama walipokuwa wakijaribu kuzima shambulio hilo.
Matukio kama haya ya uchupaji mipaka yamekuwa yakishuhudiwa katika nchi mbali mbali za Afrika. Ikumbukwe kuwa, Paul McKenzie, kiongozi wa Kanisa la Good News International Church katika eneo la Shakahola pwani ya Kenya akiwa pamoja na wenzake wanatuhumiwa kusababisha vifo vya mamia ya watu kwa kuwaamuru wajizuiye kula chakula hadi wafe kwa njaa ili waweze kukutana na Yesu Kristo huko mbinguni.