Daktari wa Rwanda jela miaka 27 kwa mauaji ya kimbari
Eugène Rwamucyo, daktari wa zamani wa Rwanda, amehukumiwa kifungo cha miaka 27 jela kwa kupatikana na hatia katika kesi ya mauaji ya kimbari ya Rwanda.
Uamuzi huo umetolewa katika Mahakama ya Paris Ufaransa. Daktari huyo amepatikana na hatia, miongoni mwa mambo mengine, ya kula njama katika mauaji ya kimbari ya Watutsi mwaka 1994. Hata hivyo, amefutiwa mashtaka ya mauaji ya kimbari na uhalifu dhidi ya ubinadamu.
Eugène Rwamucyo alianza kutumikia kifungo chake jela usiku wa Oktoba 30, 2024 kufuatia hukumu iliyotolewa na Mahakama ya Paris. Alipata wakati wa kuzungumza na familia yake na wafuasi wake wengi waliokusanyika nyuma yake kwenye chumba cha Vedel.
Amepatikana na hatia ya kula njama katika mauaji ya halaiki na kushiriki katika makubaliano ya kuandaa mauaji ya kimbari, kushiriki katika uhalifu dhidi ya ubinadamu na hatimaye kushiriki katika makubaliano ya kujiandaa kwa uhalifu huu.
Takriban watu milioni 1, wengi wao wakiwa wa jamii ya Watutsi na Wahutu wenye msimamo wa wastani, waliuawa nchini Rwanda katika mauaji ya halaiki ya Wahutu wenye misimamo mikali wakati wa mauaji ndani ya siku 100 mwaka 1994 huku dunia ikiangalia tu mauaji hayo.