Uwezekano wa kusitishwa mapigano kusini mwa Lebanon
Vyanzo vya Kizayuni, Marekani na Lebanon vimezungumzia kufikiwa makubaliano ya awali ya kusimamisha vita kusini mwa Lebanon, lakini kwamba bado kuna shaka kuhusu kiwango na njia za kufanikisha makubaliano hayo.
Mazungumzo ya kusitisha mapigano kati ya Israel na Hizbullah yamepata msukumo makubwa katika muda wa zaidi ya saa 24 zilizopita, lakini pamoja na hayo utawala wa Biden bado haujafikia makubaliano ya mwisho na Israel au Lebanon kuhusu suala hilo. Maafisa wawili wa Marekani wanaofahamu suala hilo wamedai kuwa kutokana na kuwa tayari Hizbullah kufikia makubaliano ya kusitisha mapiganom na Israel mbali na vita vya Gaza, safari ya hivi karibuni ya Amos Hochstein, mjumbe maalumu wa Biden mjini Beirut, ilifanikiwa kufikia hatua muhimu katika mazungumzo hayo.
Habari hizi kuhusu usitishaji vita unaokaribia nchini Lebanon zinatolewa huku Sheikh Naim Qassem, Katibu Mkuu mpya wa Hizbullah akisisitiza katika hotuba yake ya kwanza Jumatano jioni kwamba juhudi za kidiplomasia katika uwanja huo hazijazaa matunda yoyote hadi sasa.
Siku ya Jumatano, Hochstein alisafiri pamoja na Brett McGurk, Mshauri wa Biden katika Masuala ya Asia Magharibi huko katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu (Israel). Kabla ya hapo, Hochstein alikuwa amekutana na kuzungumza na Najib Mikati, waziri mkuu wa serikali ya Lebanon. Katika mahojiano na kituo cha televisheni cha Lebanon, Al-Jadeed, Mikati alisema kuwa Hochstein alimfahamisha kuwa "leo hali ni nzuri kuliko jana."
Rais Nicos Christodoulides wa Cyprus pia alisema baada ya kukutana na Biden katika Ikulu ya White House Jumatano kwamba anadhani makubaliano ya kusitisha mapigano nchini Lebanon yanaweza kufikiwa katika kipindi cha "wiki moja au mbili zijazo."
Matamshi hayo ya matumaini yanayotolewa na maafisa wa utawala wa Biden, pamoja na kuongezeka harakati na mashauriano ya kufikiwa makubaliano ya kusitisha mapigano, hata ikiwa ni ya muda tu, kabla ya kufanyika uchaguzi wa rais wa Marekani, ni jambo la kuzingatiwa kwa sababu kuongezeka migogoro Asia Magharibi, ambayo ilianzia kwenye vita vya Gaza na kuenea katika maeneo mengine, kumebadilisha mazingira ya uchaguzi nchini humo kwa manufaa ya Trump na chama chake cha Republican. Hivyo kusimamisha vita hata kama ni kwa muda tu, huenda kukaboresha hali ya wagombea wa chama cha Democrats na Kamala Harris katika kinyang'anyiro cha uchaguzi. Lakini swali linaloibuka hapa ni kuwa je, Warepublican na Trump watamruhusu Netanyahu kutoa fursa hiyo kwa mpinzani wake katika uchaguzi.
Kwa kuzingatia uhusiano wa karibu ulioko baina ya Netanyahu na Trump na Warepublican, haionekani kuwa Netanyahu atataka kuimarisha nafasi ya Wademocrats na mpinzani wa Trump katika uchaguzi kwa kuandaa mazingira kama hayo katika migogoro ya Asia Magharibi, isipokuwa iwapo hali kama hiyo itadhamini maslahi binafsi ya Tel Aviv na Netanyahu, au Hizbullah itoe mapiga makali ya kijeshi dhidi ya Wazayuni kiasi kwamba itamuwia vigumu Netanyahu kuendelea kubakia katika medani ya vita.
Kwa kuzingatia hayo, vyombo vya habari vya Israel viliripoti Jumatano kuwa, Amos Hochstein ambaye amehusika kuandaa rasimu ya makubaliano ya usitishaji vita, amesema kuwa: 'Netanyahu ametangaza nia yake ya kutafutia ufumbuzi vita vya Lebanon kwa namna ambayo itadhamini kurejea Wazayuni katika makazi yao.'
Jambo la kuzingatiwa hapa ni kuwa kile kinachoufanya utawala wa Kizayuni utake kuharakisha juhudi za kusimamisha vita ni maafa na hasara kubwa ambayo jeshi la Kizayuni limeipata baada ya kuanza vita vya nchi kavu nchini Lebanon na kukabiliwa na aibu ya kushindwa tena kihistoria katika ardhi ya nchi hiyo. Kuuawa askari 90 wa Kizayuni na kujeruhiwa wengine wasiopungua 750 ni sehemu tu ya maafa na hasara ambayo imelipata jeshi hilo katika kipindi hiki kifupi.
Takwimu zilizotolewa kuhusiana na maafa na hasara kubwa iliyolipata jeshi hilo zinathibitisha wazi kuwa ndoto ya utawala huo ya kutaka kulikalia tena eneo la kusini mwa Lebanon na kuunda ukanda wa usalama katika eneo hilo imegeuzwa na Hizbullah kuwa ndoto ya mchana na kuwa huenda ukashindwa na kufedheheshwa zaidi kijeshi kuliko ilivyokuwa katika vita vya siku 33 vya 2006.