Ubunifu mpya wa kisheria wa Afrika Kusini katika kuwatetea Wapalestina
(last modified Thu, 31 Oct 2024 11:06:27 GMT )
Oct 31, 2024 11:06 UTC
  • Ubunifu mpya wa kisheria wa Afrika Kusini katika kuwatetea Wapalestina

Kuendelea mauaji ya halaiki dhidi ya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza kumeifanya timu ya wanasheria wa Afrika Kusini kuwasilisha kesi inayokaribia kurasa 5,000 dhidi ya utawala katili wa Israel katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ).

Hatua hiyo ya serikali ya Afrika Kusini ni ya hivi karibuni zaidi katika faili la kesi ya jinai ambayo imewasilishwa na nchi hiyo dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel kutokana na mauaji yake ya kimbari dhidi ya Wapalestina huko Gaza. Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini amesema katika taarifa kwamba kesi kuu iliyowasilishwa ni kwamba utawala wa  Israel una "nia maalumu ya kufanya mauaji ya kimbari" dhidi ya Wapalestina.

Mawaziri wabaguzi wa rangi katika baraza la mawaziri la Netanyahu, akiwemo Itamar Ben Gvir, waziri wa usalama wa ndani wa Israel wanazungumzia waziwazi suala la kufukuza na kuwahamisha kwa nguvu Wapalestina katika Ukanda wa Gaza. Matamshi hayo yanathibitisha wazi sera za mauaji ya kizazi zinazotekelezwa na Wazayuni dhidi ya Wapalestina  huko  Gaza. Katika faili moja ya sauti, Ben Gvir  anasikika akisema: "Tumekuwa tukishambulia Ukanda wa Gaza kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa. Tunaweza kuwaambia kwamba mna fursa nyingine moja ya kuondoka hapa kwenda nchi nyingine."

Wanadiplomasia wa Afrika Kusini wanasema matamshi kama haya yanatoa ushahidi tosha na usiopingika kwamba utawala huo wa kikatili una  dhamira ya kufanya mauaji ya kizazi dhidi ya Wapalestina.

Afrika Kusini imewasilisha kesi ya mauaji ya umati dhidi ya Israel katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) mjini The Hague

Wakati serikali za Magharibi zinazodai kutetea haki za binadamu zikiwa zimekaa kimya na kutazama tu jinai hiyo ya kutisha ikitekelezwa na Wazayuni dhidi ya watu wasio na hatia huko Gaza, Afrika Kusini ikiwa ni miongoni mwa wahanga wakubwa wa ubaguzi wa rangi, imeuburuza utawala wa Kizayuni kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Haki kwa kutekeleza mauaji ya umati dhidi ya watu wa Gaza.

Majaji wa Mahakama ya Kimataifa ya Uadilifu awali walitoa uamuzi dhidi ya Wazayuni wakiwataka wasimamishe mara moja hujuma yao huko Gaza, lakini utawala huo dhalimu na waungaji mkono wake si tu kwamba wamekataa kutii  uamuazi huo bali wameushajiisha utawala huo udumishe mauaji hayo ya umati dhidi ya Wapalestina katika mwaka mmoja uliopita. Sasa viongozi wa taasisi za kimataifa na watetezi wa haki za binadamu wanazungumzia kutokea maafa ya kibinadamu katika ukanda huo.

Tedros Adhanom Ghebreyesus, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) ametoa onyo kali ikisisitiza kwamba hali ya kaskazini mwa Ukanda wa Gaza ni ya "maafa" kutokana na juhudi za jeshi la Israel za kuwafukuza wakaazi wa eneo hilo. Amesema mashambulizi makali ya Israel yanalenga kwa makusudi vituo vya afya, ambapo imekuwa vigumu kwa wagonjwa na wanaotafuta msaada kufika kwenye vituo hivyo. Vilevile ameashiria ukosefu wa vifaa muhimu vya matibabu na hivyo kupelekea watu kunyimwa huduma muhimu za afya za kuokoa maisha yao.

Rosalia Bullen, mmoja wa maafisa wa UNICEF, ameelezea hali inavyozidi kuwa mbaya mno huko  Gaza, haswa kaskazini mwa eneo hilo na kusema: "Mashambulizi ya Israel yanaongezeka kwa kasi, na hospitali na shule zinazotumiwa kama makazi salama ya wakimbizi, hazijasazwa. Afisa huyo wa UNICEF ameonya kwamba siasa za Israel kaskazini mwa Gaza zinahatarisha Wapalestina kufukuzwa katika eneo hilo." Wazayuni pia wamezuia kuingia maji, chakula na dawa katika ukanda huo. Lengo lao ni kuwalazimisha wakimbizi milioni mbili wa Kipalestina kuondoka katika Ukanda wa Gaza. Wazayuni wamewapa Wapalestina wakazi wa Gaza machaguo mawili ambayo ni ama kufa au kulazimika kuondoka katika ardhi za mababu zao.

Yahya Sinwar

Uzoefu wa jinai za kinyama ambazo zimekuwa zikitekelezwa na Wazayuni dhidi ya  Wapalestina kwa miaka 76 sasa, unaonyesha kuwa, muqawama wa Palestina hautaangamizwa kamwe na kwamba kizazi kingine kipya cha Wapalestina wenye misimamo imara na thabiti zaidi kitadhihiri kutoka kwenye magofu ya Gaza, ambacho hakitauruhusu utawala bandia wa Israel kutambuliwa rasmi duniani.

Kwa mfano, Yahya Sinwar, mmoja wa viongozi waliouawa shahidi wa harakati ya Hamas, alitoka katika kizazi cha wakimbizi wa Kipalestina waliohamia Ukanda wa Gaza. Hivi sasa amewaachia nyuma vijana wa Kipalestina taswira ya shujaa na mwanapambano shupavu wa taifa la Palestina. Bila shaka Mayahya Sinwar wengine watainuka kutoka kwenye magofu ya Gaza na kuwanyima usingizi makatili wa Kizayuni watenda jinai.

Tags