Kenya yapata Naibu Rais mpya; Profesa Kithure Kindiki
(last modified Fri, 01 Nov 2024 09:58:15 GMT )
Nov 01, 2024 09:58 UTC
  • Kenya yapata Naibu Rais mpya; Profesa Kithure Kindiki

Hatimaye Profesa Abraham Kithure Kindiki ameapishwa kuwa Naibu Rais mpya wa Kenya, kuja kurithi mikoba ya Rigathi Gachagua ambaye alibanduliwa mamlakani na Bunge la nchi hiyo mwezi uliopita wa Oktoba.

Katika hafla hiyo ya aina yake iliyofanyika katika Jumba la Mikutano la KICC jijini Nairobi, Kindiki ameapishwa na Msajili Mkuu wa Idara ya Mahakama, Winfrida Mokaya, huku Jaji Mkuu Martha Koome akishuhudia.

Rais William Ruto amehudhuria tukio hilo la kihistoria, akiwaongoza Wakenya kumpokea Kindiki kama Naibu Rais wa tatu wa nchi hiyo chini ya Katiba mpya 2010.

Kindiki akiwa ameandamana na mke wake, Dkt. Joyce Kithure, amekula viapo viwili, kiapo cha utii na kiapo cha afisi, akitangaza kujitolea kuwahudumia wananchi wote wa Kenya bila ubaguzi na upendeleo.

Akilihutibua taifa baada ya kula kiapo, Kindiki amesema, “Nimekuwa mwanafunzi wako mwema (Ruto) kwa miaka 20. Nimejifunza kuwa mnyenyekevu na mwaminifu, sitakuangusha katika majukumu mapya uliyonitwika.” 

Kindiki amepishwa huku Gachagua akiendelea kupinga mahakamani mchakato wa kuondolewa kwake madarakani 

Profesa Kindiki ambaye hadi anachukua wadhifa huu mpya alikuwa Waziri wa Mambo ya Ndani na Usalama wa Taifa ameapishwa siku moja baada ya Mahakama Kuu ya Kenya kutupilia mbali kesi zilizowasilishwa na mawakili wa Gachagua kupinga kuapishwa kwa Kindiki na mchakati wa kuondolewa madarakani Gachagua.

Gachagua alitimuliwa na Bunge la Seneti la Kenya mwezi uliopita kwa mashtaka matano kati ya 11 yaliyowasilisihwa dhidi yake na Bunge la Kitaifa, yakiwemo kuchochea migawanyiko ya kikabila na kuhujumu Idara ya Mahakama.