Machafuko yaendelea kushuhudiwa Msumbiji
(last modified Sun, 03 Nov 2024 11:42:53 GMT )
Nov 03, 2024 11:42 UTC
  • Machafuko yaendelea kushuhudiwa Msumbiji

Polisi nchini Msumbiji imetumia mabomu ya kutoa machozi na risasi za mpira kuwatawanya waandamanaji katika miji kadhaa ya nchi hiyo waliokuwa wakiandamana kupinga matokeo ya uchaguzi wenye utata.

Machafuko yamelikumba taifa hilo la Kusini mwa Afrika tangu kumalizika kwa uchaguzi mnamo Oktoba 9mwezi uliopita ambao ulikipa ushindi chama tawala cha Frelimo kilichoko madarakati tangu mwaka 1975 lakini ukilaaniwa na vyama vya upinzani vinavyodai kuwepo na udanganyifu na uchakachuaji wa matokeo.

Ripoti zinaeleza kuwa, katika mkoa wa Nampula ambao ni kitovu cha machafuko, vyombo vya usalama vilitumia nguvu kuwatawanya waandamaji wenye hasira.

Polisi haijazungumza chochote kuhusu shutuma za kutumia nguvu kupita kiasi dhidi ya waandamanaji.

Wakati huo huo, waangalizi wa uchaguzi wa Umoja wa Ulaya wamebaini "kubadilishwa bila sababu" kwa baadhi ya matokeo katika uchaguzi mkuu wa Msumbiji, huku kukiwa na shutuma za mgombea mkuu wa upinzani kwamba serikali ilimuua wakili wake.

Chama cha upinzani cha Podemos kimepinga matokeo ya uchaguzi ambayo yameonyesha kuwa chama tawala cha Msumbiji, Frelimo ambacho kimekuwa madarakani kwa nusu karne tangu uhuru,  kimeshinda.