SADC yaitisha mkutano wa dharura kuhusu mgogoro wa Msumbiji
(last modified Thu, 07 Nov 2024 06:59:32 GMT )
Nov 07, 2024 06:59 UTC
  • SADC yaitisha mkutano wa dharura kuhusu mgogoro wa Msumbiji

Ghasia za baada ya uchaguzi nchini Msumbiji kufuatia mzozo wa uchaguzi wa Oktoba 9 zimesababisha Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) kuitisha mkutano wa dharura mjini Harare wiki ijayo.

Mkutano huo uliopangwa kufanyika kuanzia Novemba 16 hadi 20, utashughulikia mzozo unaoendelea nchini Msumbiji, ambao umeibua wasiwasi mkubwa katika eneo zima la kusini mwa Afrika.

Mji mkuu wa Msumbiji, Maputo uko chini ya ulinzi mkali baada ya maandamano ya kupinga matokeo ya uchaguzi kutatiza biashara katika nchi hiyo.

Waziri wa Habari, Uenezi na Huduma za Utangazaji wa Zimbabwe, Jenfan Muswere, amewaambia waandishi wa habari mjini Harare kuwa ajenda kuu itakuwa "masuala yanayoibuka yenye umuhimu kikanda".

Zimbabwe ilichukua uenyekiti wa mzunguko wa kila mwaka wa SADC mwezi Agosti mwaka huu.

Kiongozi wa upinzani Msumbiji Venâncio Mondlane anapinga matokeo ya uchaguzi yaliyomtangaza Daniel Chapo wa Frelimo kuwa mshindi kwa kupata asilimia 70.67 ya kura.

Mondlane alisema kuwa asilimia 20.32 alizopata hazikuakisi hali halisi ya kura alizopata na kwamba kulikuwa na wizi wa kura katika uchaguzi .huo Mondlane amekimbilia Afrika Kusini.

Chama cha Madaktari cha Msumbiji (AMM) kilisema katika taarifa yake Jumanne kwamba tangu tarehe 10 Oktoba, takriban watu 16 waliuawa katika ghasia za baada ya uchaguzi huku 108 wakijeruhiwa.