Baraza la Usalama lawaweka vikwazo viongozi wawili wa RSF nchini Sudan
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limewawekea vikwazo viongozi wawili wa Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) nchini Sudan, kwa madai kwamba wanavuruga usalama wa nchi hiyo kupitia ghasia na ukiukaji wa haki za binadamu.
Kamati ya Vikwazo ya UN, ambayo inajumuisha wanachama 15 wa Baraza la Usalama, imeidhinisha pendekezo lililowasilishwa mwishoni mwa Agosti mwaka jana la kuwekwa marufuku ya kusafiri na kuzuiliwa mali za Kamanda wa Operesheni wa wapiganaji wa RSF, Osman Mohamed Hamid Mohamed, na kamanda wa kundi hilo huko Darfur Magharibi, Abdulrahman Juma Barakallah.
Shirika la habari la Reuters limeripoti kuwa, hivi ni vikwazo vya kwanza vilivyowekwa na Umoja wa Mataifa katika vita vya sasa nchini Sudan, vilivyozuka Aprili 2023 kati ya jeshi la taifa linaloongozwa na mkuu wa Baraza la Utawala na mtawala mkuu wa nchi hiyo, Abdel Fattah al-Burhan, na Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) vinavyoongozwa na naibu wake wa zamani, Mohamed Hamdan Dagalo (Hemedti).
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilianzisha mfumo wa vikwazo kwa Sudan mwaka 2005 katika jaribio la kumaliza mzozo wa Darfur.
Vita vya sasa nchini Sudan vimesababisha wimbi la ghasia za kikabila, ambazo kwa kiasi kikubwa zinahusishwa na kundi la RSF, ambalo kwa upande wake linakanusha kuwadhuru raia na kulituhumu jeshi la taifa.
Umoja wa Mataifa unasema kuwa takriban watu milioni 25 - nusu ya wakazi wa Sudan - wanahitaji msaada kutokana na kuenea kwa njaa katika kambi za wakimbizi na kukimbia kwa watu milioni 11 kutoka kwenye makazi yao, na karibu milioni 3 kati yao wamekimbilia nje ya nchi.