Wanaharakati: Itakuwa bora iwapo Trump atapuuza nchi za Afrika
Wanaharakati Afrika wamesema sera ya mambo ya nje ya Marekani haina faida kwa bara la Afrika na wala haileti maendeleo katika bara hilo na hivyo iwapo rais mteule wa Marekani Donald Trump atapuuza uhusiano na Afrika hilo litakuwa kwa maslahi ya bara hilo
Sheriff Ghali Ibrahim, mwanamajumuiya wa Afrika ameliambia Shirika la Habari la Sputnik kwamba kutokana na mabadiliko ya hali ya kimataifa, nchi za Afrika zimeimarisha uhusiano na muungano unaoibuka wa BRICS.
Amesema anatumai kwamba Rais mteule wa Marekani Donald Trump ataendelea kuipuuza Afrika kwa sababu iwapo Marekani itaanza kuelekeza nguvu zake katika bara hilo, basi itasababisha matatizo katika bara hilo.
Naye mwanaharakati mwingine wa kijamii Nathalie Yamb ameunga mkono kauli hiyo katika mahojiano na Sputnik kando ya Mkutano wa kwanza wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya Russia na Afrika katika mji wa Sochi nchini Russia.
Amesema Afrika itakuwa karika hali bora zaidi kama Marekani itajikita katika ile sera ya Trump ya "kuifanya Marekani kuwa Kubwa Tena", kwani yamkini ikifanya hivyo haitakuwa na wakati wa kuingilia mambo ya ndani ya Afrika.
Yamb amesema ni wazi kuwa Trump si rafiki wa Afrika na kuongeza kuwa pamoja na hayo, mfumo wa serikali ya Markeani umepangwa kwa njia ambayo rais hana mamlaka yote na hivyo kuna uwezekano Marekani ikaendelea kuingilia mambo ya Afrika.
Wakati wa urais wake, Trump alilitazama Afrika kama bara la kupuuzwa au kunyonywa inapofaa. Ikumbukwe kuwa wakati akiwa rais, Trump aliwahi kuzifananisha nchi za Afrika, Haiti, Ecuador na 'Shimo la Choo'.