Serikali ya Niger yalifutia leseni shirika jingine la mkoloni Ufaransa
Utawala wa kijeshi nchini Niger umetangaza kuwa, umefuta leseni ya shirika lisilo la kiserikali la Acted la Ufaransa kufanya kazi nchini humo, katikati ya mvutano na mkoloni wake huyo wa zamani.
Wizara ya Mambo ya Ndani ya Niger imetoa taarifa hiyo, bila ya kubainisha sababu za kufuta leseni hiyo. Shirika jingine la APBE pia lilikumbwa na kalamu hiyo nyekundu ya utawala wa Niger ya kufutiwa leseni.
Shirika la Acted limekuwa ikifanya kazi nchini Niger tangu 2009, likijishughulisha zaidi na watu waliokimbia makazi yao katika taifa hilo la Afrika Magharibi lililokumbwa na ghasia za waasi.
Tangu utawala wa kijeshi ulipoingia madarakani Julai 2023 huko Niger, ulianza kuipa kisogo Ufaransa, na kuanzisha uhusiano na wanaharakati wenzao Burkina Faso na Mali, pamoja na Russia.
Juni mwaka huu pia, Niger ilibatilisha kibali cha shirika la Orano la nishati la Ufaransa kuendelea kuzalisha fueli nyuklia katika moja ya migodi mikubwa zaidi ya urani duniani.
Uhusiano wa Niger na Ufaransa uliharibika zaidi Julai mwaka jana, baada ya jeshi kumpindua rais ambaye wananchi wa Niger walikuwa wanalalamika vikali kwamba ni kibaraka mkubwa wa Ufaransa, Mohammad Bazoum.