Iran, Russia na Uturuki zalaani jinai za Wazayuni dhidi ya Wapalestina
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Russia na Uturuki zimetoa taarifa ya pamoja zikilaani jinai za Wazayuni dhidi ya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza na mashambulizi ya utawala huo ghasibu dhidi ya Lebanon na Syria.
Iran, Russia na Uturuki jana Jumanne zilitaja hatua za kichokozi za Israeli katika eneo Magharibi mwa Asia kuwa ni ukiukaji wa sheria za kimataifa. Nchi hizo tatu zimeeleza haya katika fremu ya mazungumzo ya Astana kuhusu Syria.
Iran, Russia na Uturuki pia zimesisitiza udharura wa kuchukuliwa hatua kuhusu mifumo ya Umoja wa Mataifa ili kuwasaidia wakimbizi wa Lebanon huko Syria ambao wamehamia huko baada ya kushtadi mapigano. Nchi hizo tatu pia zimesisitiza umuhimu wa kuendelezwa juhudi za kuhuisha uhusiano kati ya Ankara na Damascus.
Iran, Russia na Syria vilevile zimesema kuwa zinapinga kuporwa na kuhamishwa kinyume cha sheria mafuta na rasilimali nyingine ambazo zinapasa kuwa mali ya wananchi wa Syria.
Iran, Russia na Uturuki pia zimekubaliana kufanya mkutano wa 20 wa "Mchakato wa Astana" huko Russia katika nusu ya kwanza ya mwaka ujao wa 2025.