Viongozi wa Jumuiya ya SADC kujadili machafuko ya Msumbiji
(last modified Fri, 15 Nov 2024 11:15:12 GMT )
Nov 15, 2024 11:15 UTC
  • Viongozi wa Jumuiya ya SADC kujadili machafuko ya Msumbiji

Viongozi wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika SADC wanatarajiwa kukutana mwishoni mwa juma hili, katika mji mkuu wa Zimbabwe Harare kwa minajili ya kujadili mzozo wa Msumbiji.

Siku ya Jumatano, watu wawili waliripotiwa kuuawa mjini Maputo baada ya polisi kujaribu kuyazima maandamano ya upinzani huku mpaka wa nchi hiyo na Afrika Kusini ukifungwa.

Ghasia hizo ziliikumba katika nchi hiyo ya kusini mwa Afrika baada ya uchaguzi wa rais wa Oktoba 9, ambapo Tume ya Taifa ya Uchaguzi ilitangaza kuwa, Daniel Chapo wa chama tawala cha Mozambique Liberation Front (Frelimo) ameshinda kwa asilimia 70 ya kura, lakini wapinzani wamekataa kutambua matokeo hayo. Kiongozi wa upinzani, Venancio Mondlane, ambaye kwa mujibu wa tume hiyo ameshika nafasi ya pili kwa asilimia 20.32 ya kura ameendelea kutoa mwito wa kupinga matokeo hayo akiyataja kuwa ni ya udanganyifu.

Mrengo wa upinzani unasema kuwa matokeo yamechakachuliwa na kukipendelea chama tawala cha FRELIMO. Mataifa mbalimbali ikiwemo Afrika Kusini yametoa wito wa kurejeshwa hali ya utulivu na utawala wa sheria nchini Msumbiji.