Afrika Kusini yatangaza maafa ya taifa kutokana na mafuriko na kimbunga
(last modified Fri, 15 Nov 2024 12:07:50 GMT )
Nov 15, 2024 12:07 UTC
  • Afrika Kusini yatangaza maafa ya taifa kutokana  na mafuriko na kimbunga

Serikali ya Afrika Kusini imetangaza hali ya maafa ya taifa zima kufuatia mafuriko makubwa na kimbunga kilichosababisha uharibifu mkubwa wa mali na vifo vya watu katika majimbo saba kati ya tisa ya nchi hiyo.

Elias Sithole, mkuu wa Kituo cha Taifa cha Kudhibiti Majanga cha Afrika Kusini, ametangaza janga la taifa zima akisisitiza kuwa maafa yaliyosababishwa na hali hiyo mbaya ya hewa ni makubwa. 

Katika taarifa yake, Sithole amesema: "Mvua kubwa, mafuriko, upepo mkali na mvua ya mawe ni matukio ya kimaumbile yaliyoanzia Oktoba 22 na kuendelea hadi Oktoba 29 na yamesababisha maafa makubwa katika majimbo ya Eastern Cape, KwaZulu-Natal, Free State, Limpopo, Kaskazini Magharibi, Gauteng na Mpumalanga."

Amesema: "Hali mbaya ya hewa imesababisha watu kupoteza maisha, uharibifu wa mali, uharibifu wa miundombinu na mazingira pamoja na kukatika huduma za msingi kama umeme na maji."

Maafisa wa Afrika Kusini wasema mafuriko yamesababisha maafa makubwa nchini humo

 

Vyombo vya habari vya ndani ya Afrika Kusini vimetangaza kuwa, kimbunga na mafuriko hayo yamesababisha vifo vya takriban watu 10 na kuwafanya mamia wengine kuyahama makazi yao katika mkoa wa Eastern Cape pekee.

Akitangaza hali ya maafa ya taifa, Sithole amesema: "Baada ya kutathmini ukubwa na ukali... Nimekuja mbele yenu kutangaza maafa ya taifa kutokana na hali mbaya ya hewa iliyokumba nchi yetu." 

Tangazo la maafa ya taifa litaruhusu serikali kuu ya Afrika Kusini kuyapa pesa za dharura majimbo yaliyoathiriwa na kuyawezesha kushughulikia uharibifu uliosababishwa na mafuriko hayo.