Mamilioni ya Wasenegal wameelekea vituo vya kupigia kura kuchagua Bunge jipya
Wasenegal leo wamepiga kura katika uchaguzi wa Bunge ambao utaamua kama rais mpya wa nchi hiyo Bassirou Diomaye Faye ataweza kufanya mageuzi makubwa aliyokusudia au la.
Wapiga kura nchini Senegal leo wamechagua wabunge 165 wa bunge la taifa hilo, ambapo kwa sasa, chama cha Rais Faye hakijaweza kuwa na viti vingi zaidi.
Orodha 41 za wagombea, zinazojumuisha miungano minne mikuu zimejitosa kwenye kinyang'anyiro hicho. Rais wa zamani Macky Sall anaongoza jukwaa la upinzani la Takku Wallu lenye viti vingi bungeni.
Rais Faye ambaye alichaguliwa mwezi Machi amesema, jukwaa hilo limemzuia kutekeleza mageuzi aliyoahidi wakati wa kampeni za uchaguzi wa rais, ikiwa ni pamoja na kupambana na ufisadi, kupitia upya vibali vya uvuvi kwa makampuni ya kigeni, na kutenga fungu kubwa zaidi la mapato ya maliasili za nchi kwa faida ya wananchi.
Waziri mkuu wake Ousmane Sonko hakuhudhuria katika bunge hilo ambapo upinzani ulitishia kumpigia kura ya kutokuwa na imani naye.
Wanasiasa walihitimisha kampeni za uchaguzi zilizotawaliwa na mvutano siku ya Ijumaa Novemba 15. Kampeni hizo ziliambatana na mapigano ya hapa na pale kati ya wafuasi wa vyama tofauti.
Kwa mujibu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Senegal, mapigano yalizuka kati ya wafuasi wa vyama katikati mwa nchi katika wiki za hivi karibuni na makao makuu ya chama cha upinzani yalichomwa moto katika mji mkuu Dakar.
Siku ya Jumanne Novemba 12, waziri mkuu Sonko aliyewahi kuwa pia kiongozi maarufu wa upinzani aliyesaidia kufanikisha ushindi wa Rais Faye, alishutumu mashambulizi yaliyofanywa dhidi ya wafuasi wa chama chake cha PASTEF huko Dakar na katika miji mingine.
Mwezi uliopita gari la Sonko lilishambuliwa kwa mawe makabiliano yalipozuka kati ya wafuasi wake na washambuliaji wasiojulikana alipokuwa akifanya kampeni mjini Koungueul, katikati mwa nchi.
Mnamo mwezi Septemba, Rais wa Senegal alivunja bunge lililohodhiwa na upinzani, na hivyo kufungua njia ya kufanyika uchaguzi wa mapema.../