Jul 24, 2016 13:30 UTC
  • Jeshi la Nigeria laahidi kukomboa maeneo yanayodhibitiwa na Boko Haram

Jeshi la Nigeria limetangaza kuwa, litaendeleza operesheni zake hadi kuyakomboa maeneo yote yanayodhibitiwa na wanachama wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram nchini humo.

Lucky Ilabor, Kamanda wa ngazi ya juu wa kikosi maalumu cha jeshi la Nigeria kaskazini mashariki mwa nchi hiyo, ameyasema hayo katika kikao cha waandishi wa habari ambapo sanjari na kuashiria kutoweka askari 19 na wapiganaji wa kujitolea katika hujuma ya kushtukiza ya wanachama wa Boko Haram katika eneo la jeshi huko Maiduguri, amesisitiza kuwa, kundi hilo litalipa gharama kubwa kwa kitendo chake hicho.

Askari wa Nigeria katika operesheni zao dhidi ya Boko Haram

Katika shambulizi hilo la kushtukiza lililotokea siku ya Alkhamis, wanamgambo hao waliwateka nyara askari 19 wa nchi hiyo na kutoweka nao.

Ripoti zinasema wakati wanachama wa kundi hilo walipokuwa wakiwateka nyara askari hao walisikika wakisema kuwa, wametekeleza shambulizi hilo kujibu operesheni ya askari wa serikali dhidi ya moja ya ngome za Boko Haram katika eneo la Alagarno lililopo katika jimbo la Yobe. Afisa mmoja wa jeshi la Nigeria amesema kuwa, askari hao walitekwa nyara wakati walipokuwa wakirejea kambini. Lucky Ilabor amesema kuwa, kwa sasa jeshi hilo likishirikiana na Wizara ya Ulinzi linafanya juhudi ya kuwatambua na kuwanasa wanachama wa kundi hilo la kigaidi. Amefafanua kuwa, katika mapigano hayo askari walifanikiwa kuwaangamiza wapiganaji kadhaa wa Boko Haram sanjari na kudhibiti gari moja la lililokuwa na kombora la anga.

Askari wa Nigeria

Kabla ya hapo pia polisi ya Nigeria ilitangaza kuwa, katika hujuma ya wanachama wa genge hilo katika jimbo la Borno, kwa akali raia saba waliuawa. Taarifa hiyo ilisisitiza kuwa, wafuasi wa Boko Haram wamesababisha hasara kubwa kwenye makazi ya raia wa eneo hilo, ambapo pia walipora mali za raia hao. Mwezi uliopita, Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria katika hatua za kukabiliana kwa dhati na vitisho wa kundi hilo la kigaidi alimteua Muhammad Osman, kuwa mkuu mpya wa Idara ya Intelejensia na Ulinzi nchini humo. Weledi wa mambo waliitafsiri hatua hiyo ya Rais Buhari kuwa ina lengo la kubadili kikamilifu siasa za nchi hiyo katika vita dhidi ya Boko Haram na badala yake kujikita zaidi katika kukusanya taarifa za kiupelelezi katika njia ya kukabiliana na vitisho vya kiusalama vya wanachama wa kundi hilo. Kwa mujibu wa ripoti rasmi, Nigeria ni nchi ya nne duniani yenye mgogoro mmkubwa na idadi kubwa ya watu waliouawa na kujeruhiwa katika mapigano yaliyojiri mwaka 2015 uliopita baada ya Syria na Yemen.  

Operesheni za kuwasaka wanamgambo wa Boko Haram

Ofisi ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa (OCHA) imeielezea hali ya mambo huko kaskazini mashariki mwa Nigeria kuwa ni mbaya sana huku wakimbizi wa maeneo hayo wakikabiliwa na njaa kali. Taarifa ya ofisi hiyo inasema, endapo hatua za kuboresha hali ya kibinaadamu hazitachukuliwa ktika eneo la kaskazini mashariki mwa nchi, basi mamia ya watu watapoteza maisha kutokana na njaa kali.

Katika fremu hiyo Umoja wa Mataifa umetangaza habari ya kufika msaada wa kwanza wa chakula wa umoja huo kwenye mji wa Banki, kaskazini mwa Nigeria karibu na mpaka wa Cameroon. Ofisi ya Uratibu wa Masuala ya Kibinaadamu ya Umoja wa Mataifa imetangaza kuwa, karibu aina 30 ya vyakula vimetumwa kupitia mpaka wa nchi jirani ya Cameroon kwenda mji wa Banki, ambao wakimbizi waliopo eneo hilo wanakabiliwa na njaa kali. Chakula hicho kitagawiwa kwa wakimbizi elfu 25 ambao waliyakimbia makazi yao kutokana na mashambulizi ya wanachama wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram. Aidha ripoti hiyo imesema kuwa, hivi karibuni jumla ya kilo 700 za chakula zimetumwa kwa ndege kwenda mji wa Maiduguri kwa ajili ya watoto wanaokabiliwa na utapiamlo katika jimbo la Borno, kaskazini mashariki mwa Nigeria.

Inafaa kukumbusha kuwa, mashambulizi ya kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram yalianza mwaka 2009 huko kaskazini mashariki mwa nchi hiyo na tangu wakati huo zaidi ya watu 20, 000 wameuawa na zaidi ya wengine milioni mbili na laki sita kuwa wakimbizi.

Tags