Feb 14, 2020 02:41 UTC
  • Maelfu ya Wacameroon wakimbilia Nigeria wakiepa kushtadi machafuko nchini kwao

Wakimbizi raia wa Cameroon karibu elfu nane wamekimbilia katika maeneo ya mashariki na kusini mwa Nigeria katika kipindi cha wiki mbili zilizopita. Hayo yalielezwa jana Alhamisi na Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa.

Shirika la UNHCR limesema kuwa idadi jumla ya Wacameroon waliokimbilia Nigeria hadi sasa imefikia elfu 60,000.

Mzozo kati ya jeshi la Cameroon na wanamgambo wanaozungumza lugha ya Kingereza wanaopigania kujitenga na kuasisi nchi yao kwa jina la Ambazonia ulianzia baada ya serikali ya Cameroon kuwakandamiza vikali raia waliokuwa wakiandamana kwa amani wakilalamikia kitendo cha kudunishwa kwao na jamii ya waliowengi wa nchi hiyo wanaozungumza lugha ya Kifaransa.

Mzozo huo wa Cameroon umepelekea raia laki tano kuyahama makazi yao. Weledi wa masuala ya kisiasa wanasema kuwa hiyo ni changamoto kuu inayomkabili Rais Paul Biya  ambaye amekuwa madarakani huko Cameroon kwa karibu miaka 40 sasa. 

Rais Paul Biya wa Cameroon 

Hali za raia hao wa Cameroon wanaoikimbia nchi yao wakielekea Nigeria imetajwa kuwa mbaya. Baadhi yao wameshuhudiwa wakiwasili mipakani wakiwa na majeraha ya risasi. Habari zinasema kuwa, wengi kati yao wametoka katika maeneo karibu na mipaka na wametaabika pakubwa kufika Nigeria kwa kuvuka misitu na mapori.

Tags