Apr 27, 2019 02:42 UTC
  • Madaktari waruhusiwa kumfanyia uchunguzi wa kiafya Sheikh Ibrahm Zakzaky

Hatimaye timu ya madaktari imeruhusiwa kumfanyia uchunguzi wa kiafya Sheikh Ibrahim Zakzaky, Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria ambaye angali anashikiliwa kizuizini.

Kanali ya Televisheni ya Press TV imeripoti kwamba, timu ya madaktari wa shirika lisilo la kiserikali la Kamisheni ya Haki za Binadamu ya Kiislamu yenye makao yake nchini Uingereza inatarajiwa kumpima na kumfanyia uchunguzi wa kiafya Sheikh Ibrahim Zakzaky.

Taarifa ya kamisheni hiyo imeeleza kwamba, ina matumaini hatua hiyo itapelekea kufahamika bayana hali ya kiafya ya kiongozi huyo wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria.

Ripoti zinaeleza kwamba, tangu Sheikh Ibrahim Zakzaky alipotiwa mbaroni na kushikiliwa kizuizini mwaka 2015, hajawahi kufanyiwa uchunguzi wa kitiba licha ya kuwa, amekuwa akisumbuliwa na majeraha.

Mwezi uliopita Sheikh Ibrahim Zakzaky alishindwa kufika mahakamani kuhudhuria kesi yake kutokana na kudorora hali yake ya afya.

Sheikh Ibrahim Zakzaky, Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria

Sheikh Ibrahim Zakzaky na mkewe walikamatwa na kuwekwa kizuizini tarehe 13 Desemba 2015, wakati askari wa jeshi la Nigeria walipovamia na kufanya hujuma dhidi ya Hussainiyyah ya mji wa Zaria katika jimbo la Kaduna kaskazini mwa nchi hiyo, ambapo mamia ya Waislamu waliuawa shahidi.

Mnamo mwezi Desemba 2016, Mahakama Kuu ya Nigeria ilitoa hukumu ya kutaka Sheikh Zakzaky aachiwe huru mara moja, sambamba na kulitaka jeshi na vyombo vya usalama viilipe familia yake fidia ya dola laki moja na nusu, lakini si tu vimekaidi kutekeleza hukumu hiyo ya mahakama lakini vimeendelea pia kumweka kizuizini mwanaharakati huyo pamoja na mkewe.

Tags