Rais Samia: Tumepoteza wenzetu 13 Kariakoo
(last modified Mon, 18 Nov 2024 03:30:34 GMT )
Nov 18, 2024 03:30 UTC
  • Rais Samia: Tumepoteza wenzetu 13 Kariakoo

Watu 13 wamethibitika kufariki dunia na wengine 84 kujeruhiwa kufuatia ajali ya kuporomoka kwa jengo katika eneo la Kariakoo mkoani Dar es Salaam, iliyotokea juzi Jumamosi Novemba 16.

Rais Samia Suluhu Hassan wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amesema kuwa idadi hiyo ya vifo ni pamoja na majeruhi ni ya hadi saa nne asubuhi jana Jumapili Novemba 17, 2024.

Rais Samia ametoa idadi hiyo alipokuwa akitoa salamu za pole kwa waathirika wa ajali ya kuporomoka kwa  jengo hilo la ghorofa huko Kariakoo juzi Jumamosi.

Majeruhi wakiondolewa katika jengo lililoporomoka Kariakoo, Dar es Salaam 

Ametoa salamu hizo jana Jumapili akiwa katika mji wa  Rio de Janeiro nchini Brazil  kwaajili ya kushiriki katika Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Nchi Wanachama wa Kundi la G20 uliopangwa kuanza leo Novemba 18, 2024. 

Akilihutubia taifa kutokea Brazil, Rais Samia alisema kuwa  na  hapa ninamnukuu  "nimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya kuporomoka kwa ghorofa Kariakoo Dar es salaam. Nimekuwa nikipata taarifa za mara kwa mara kutoka kwa Waziri Mkuu  kuhusu mwenendo wa zoezi la uokoaji na ninaendelea kufuatilia zoezi hilo kwa ukaribu zaidi.  Amesema majeruhi 26 wanaendelea na matibabu na kwamba watu 13 wamepoteza maisha. Amesema kuwa, serikali itabeba gharama za matibabu kwa wote waliojeruhiwa na kuhakikisha waliofariki wanasitiriwa ipasavyo", amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.