Siku ya Utamaduni wa Washirazi yaadhimishwa nchini Tanzania
Balozi wa Iran nchini Tanzania ameshiriki katika Siku ya Utamaduni wa Washirazi iliyofanyika jijini Dar es Salaam ili kuzidi kutia nguvu uhusiano wa kiudugu ulipo baina ya Iran na Tanzania.
Habari hiyo imetangazwa na Taasisi ya Utamaduni na Mahusiano ya Kiislamu ya Iran ambayo imesema kuwa, Balozi wa Iran nchini Tanzania, Hosein Alvandi ameshiriki kwenye sherehe hizo zilizofanyika jana Jumatatu jijini Dar es Salaam na kusema kuwa, uhusiano wa nchi hizi mbili unazidi kuimarishwa na uwepo uliojaa fakhari wa Washirazi nchini Tanzania. Amehimiza kufanyika jitihada zaidi za kuhakikisha uhusiano huo unakuwa imara zaidi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Utamaduni cha Iran nchini Tanzania, Mohsen Moarefi amezungumzia miamala na mahusiano mazuri sana yaliyojitokeza baada ya Washirazi wa Iran kuelekea mashariki mwa Afrika na kusisitiza kuwa, mlahaka wa Wairan unatofautiana kikamilifu na wa wakoloni wa Magharibi ambao walizivamia nchi za Afrika ili kupora utajiri wao na hadi sasa wanajali tu maslaini yao binafsi.
Ameongeza kuwa, kutokana na Washirazi kuoanisha ada na desturi zao na mila na desturi za wenyeji wa Afrika Mashariki, wameweza kuja na utamaduni mpya wa kipekee ambao hadi leo hii wakazi wa mashariki mwa Afrika wanajivunia nao.
Wazungumzaji wengine waliohudhuria sherehe hizo nao pia wamegusia uhusiano wa kihistoria baina ya wananchi wa Iran na Waswahili wa mashariki mwa Afrika na kutilia mkazo wajibu wa kutunzwa na kuendelezwa suala hilo.