Khartoum yakosoa uingiliaji wa Imarati katika masuala ya ndani ya Sudan
Wizara ya Ulinzi ya Sudan imetoa taarifa ikikosoa uingiliaji wa Imarati katika masuala ya ndani ya nchi hiyo na pia hatua yake ya kuwapatia silaha na zana za kijeshi wanamgambo wa Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF).
Sudan imesema kuwa Imarati (UAE) imewapa wapiganaji wa RSF cha Sudan silaha za kisiasa zikiwemo droni za kistratejia na makombora yanayoongozwa kutokea mbali. Itakumbukwa kuwa RSF inapigana na jeshi la Sudan.

Brigedia Ahmed Saleh Aboud, msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya Sudan amesema katika mkutano na waandishi wa habari kwamba Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) umetuma ndege zisizo na rubani moja kwa moja katika uwanja wa ndege wa Umm -Jarass huko Chad na kuzikabidhi kwa wanamgambo wa RSF.
Msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya Sudan ameongeza kuwa wataalamu kutoka UAE pia wanasimamia mafunzo ya mamluki na wanamgambo wengi wa RSF ndani ya Sudan katika maeneo ya Khartoum na huko Darfur.
Yassin Ibrahim, Waziri wa Ulinzi wa Sudan pia amesema kuhusu hatua ya Imarati ya kukipatia silaha kikosi cha RSF kwamba: Huu ni uadui wa wazi wa Imarati; na Sudan ina haki ya kujibu hatua hii dhidi kwa wakati na mahali mwafaka.