Polisi ya Malawi yamkamata 'Fisi' aliyenajisi watoto, Rais Mutharika aamuru achunguzwe
(last modified Tue, 26 Jul 2016 16:55:28 GMT )
Jul 26, 2016 16:55 UTC
  • Polisi ya Malawi yamkamata 'Fisi' aliyenajisi watoto, Rais Mutharika aamuru achunguzwe

Polisi ya Malawi imemtia nguvuni 'fisi' aliyekuwa akiwanajisi watoto wadogo kwa madai ya kuwasafisha au kuwafanyia tambiko la kimila na kiutamaduni.

Bwana Eric Aniva amekamatwa kufuatia amri ya Rais Peter Mutharika wa Malawi ya kukamatwa kwake baada ya kukiri kwamba amefanya ngono na watoto wadogo zaidi ya 100 kwa kulipwa fedha na wazazi wao, ikiwa ni sehemu ya utamaduni wa jamii moja ya kusini mwa nchi hiyo.

Amri hiyo imetolewa baada ya Bwana Eric Aniva  wa wilaya ya Nsanje kukiri kwamba, amefanya ngono na wasichana wadogo kwa kulipwa fedha ambazo ni sawa na kati ya dola nne na saba za Marekani kwa kumbikiri kila mtoto mmoja.

Rais Peter Mutharika wa Malawi

Rais wa Malawi amesema ametoa amri ya kukamawa Bwana Eric Aniva, kumsaili na kumpandisha kizimbani kwa kuwanajisi watoto wadogo.

Vilevile imebainika kuwa Bwana Eric Aniva aliyewanajisi watoto hao wadogo ni mwathirika wa virusi vya HIV.

Ripoti zinasema jamii hiyo ya kusini mwa Malawi imekuwa na utamaduni wa kukabidhi watoto wao wa kike wenye umri wa kati ya miaka 11 na 14 wakati wa hedhi yao ya kwanza, kwa mtu anayejulikana kwa jina la 'fisi ili abikiriwe wakiwa na imani kwamba, ubikira ni mkosi na kwamba kitendo hicho kinawasafisha watoto hao.

Watu wa jamii hiyo hufanya sherehe kubwa inayomtangulia binti akipelekwa unyagoni kisha kuwatembelea shangazi wake kabla ya kukabidhiwa kwa kwa fisi.

Vitendo viovu kama hivyo vya eti kusafishwa au kufanyiwa tambiko huwa vinafanywa pia kwa wanawake wanaofiwa na waume zao ili eti waondolew mkosi na vilevile wanawake wanaoavya mimba.