Senegal; kituo kinachofuata cha kufukuzwa wanajeshi wa Ufaransa barani Afrika
Ousmane Sonko,Waziri Mkuu wa Senegal amewaambia wabunge wa nchi hiyo kwamba wanajeshi wa Ufaransa lazima waondoke nchini humo na kwamba, kambi za kijeshi za kigeni katika nchi hiyo ya Kiafrika zitafungwa katika siku za usoni.
Sonko amesema, nchi hiyo itafunga kambi zote za kijeshi za kigeni ikiwa ni sehemu ya juhudi za serikali za kupitia upya sera ya ulinzi na kuimarisha mamlaka ya kitaifa. Sonko alitangaza uamuzi huo katika Bunge la Taifa juzi Jumamosi wakati wa uwasilishaji sera kuu, ambapo alielezea mkakati wa mabadiliko ya taifa hilo la Afrika Magharibi katika miaka 25 ijayo.
Rais wa Senegal Bassirou Diomaye Faye, ambaye amekuwa madarakani kwa muda wa chini ya mwaka mmoja, alitangaza kwa mara ya kwanza uamuzi wake wa kuondoa jeshi la Ufaransa nchini mwake katika mahojiano na shirika la habari la AFP mwishoni mwa mwezi uliopita. Alisema kambi za jeshi la Ufaransa "hazikidhi" kulindwa mamlaka ya kujitawala ya nchi hiyo ya Afrika Magharibi.
Rais wa Senegal alisema katika sehemu nyingine ya mahojiano yake hayo: Sisi tunashirikiana na Marekani, China na Uturuki bila ya nchi hizo kuwa na kambi za kijeshi katika ardhi yetu. Je, Ufaransa inaweza (kukubali) hali kama hiyo? Je, hii si kwa sababu Wafaransa wamekuwa Senegal tangu kipindi cha utumwa na haiwezekani kufanya vinginevyo?
Senegal ndiyo kituo cha mwisho cha ushawishi wa moja kwa moja wa Ufaransa katika kanda ya Afrika Magharibi, na takriban kuna wanajeshi 500 wa Ufaransa, wanaojumuisha wakufunzi na washauri. Baada ya Niger, Mali na Burkina Faso, taifa la Senegal ni nchi ya nne barani Afrika iliyoamua kuwafukuza wanajeshi wa Ufaransa. Serikali ya Chad ilitangaza tarehe 28 Novemba kwamba, imefuta makubaliano yake ya kijeshi na serikali ya Ufaransa kuhusu uwepo wa wanajeshi 1,000 wa Ufaransa nchini humo.
Filihali Ufaransa ina kambi za kudumu za kijeshi nchini Djibouti, Chad, Gabon, Ivory Coast na Senegal. Kuna wanajeshi 1,500 nchini Djibouti, 1,000 nchini Chad, 600 nchini Ivory Coast, na 500 nchini Gabon na Senegal. Chad imetangaza kusitisha ushirikiano wake wa kijeshi na Ufaransa. Takriban wanajeshi 4,000 kati ya 10,000 wa Ufaransa walioko Afrika (katika miaka 5 iliyopita) wamesalia barani humo, na inatarajiwa kwamba idadi hii itapungua hadi chini ya askari 2,000 katika miezi michache ijayo kufuatia matangazo ya hivi karibuni ya Chad na Senegal ya kuwatimua wanajeshi wa mkoloni huyo wa zamani.
Ufaransa ilikoloni nchi ishirini za Kiafrika kwa miongo kadhaa. Baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia na wimbi la uhuru wa makoloni ya wakoloni wa Ulaya, mkoloni huyu wa Ulaya alijaribu kudumisha ushawishi wake barani Afrika na uwepo wa kijeshi katika baadhi ya makoloni yake ya zamani. Ingawa Ufaransa inajiona kuwa chimbuko la demokrasia, lakini ilifanya njama za kudumisha satwa yake ya kijeshi na kiuchumi barani Afrika kwa kuunga mkono serikali za kidikitea ambazo ni makoloni yake ya zamani.
Gazeti la Uhispania la El Pais limeandika: Serikali nyingi katika nchi za Kiafrika ambazo zilikuwa makoloni ya Ufaransa zilitia saini makubaliano na mataifa wakoloni wa zamani ili kuhakikisha zinapata dhamani ya kubakia madarakani dhidi ya waasi wapinzani na mapinduzi. Kwa njia hii, Ufaransa, ikiwa na wanajeshi 10,000 pekee katika nchi tofauti za Kiafrika, iliweza kuingilia kijeshi mara 30 kati ya miaka ya 1964 na 2012.
Baada ya utulivu wa serikali barani Afrika, serikali za Afrika zikiwa katika njia ya matukio ya kimataifa zimechukua mkondo wa ukuaji na maendeleo na zinafuatilia kutumia fursa za kiwango cha juu zaidi kwa ajili ya ustawi na maendeleo. Mataifa ya Afrika hayataki tena kufuata njia ya wakoloni wa zamani ya Ulaya katika uhusiano wao na ulimwengu. Serikali za Kiafrika zinafuatilia uhusiano wenye uwiano na nchi zote za dunia.
Wakati kulipoanza vita vya Russia na Ukraine, dola la Marekani na serikali za Ulaya zilijaribu kuzishinikiza serikali za Kiafrika zifuate mtazamo wao katika kuiwekea vikwazo Russia, lakini serikali za Afrika zilikataa matakwa hayo na badala yake zikajaribu kuchukua msimamo huru katika vita vya Ukraine.
Katika uga wa kimataifa pia bara la Afrika linafanya hima ya kuwa na sauti huru duniani. Enzi za serikali dhalimu zinazoungwa mkono na wakoloni wa Ulaya zimepita na kumalizika. Wakati wa ziara yake nchini Djibouti akiwa mwenyeji wa moja ya vituo vya mwisho vya kijeshi vya Ufaransa, Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron alikiri wazi mabadiliko haya na kusema: Afrika inabadilika kwa sababu maoni ya umma na Serikali yamo katika hali ya kubadilika, hivyo nafasi yetu barani Afrika pia itabadilika.