AU na nchi kadhaa za kikanda zakaribisha usitishaji vita Gaza
Nchi kadhaa za Kiafrika na Umoja wa Afrika (AU) zimekaribisha makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya Israel na Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas).
Moussa Faki Mahamati, Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika amesema anapongeza mchango uliotolewa na Qatar na nchi nyingine kadhaa katika kufanikisha makubaliano hayo na kwamba AU inatoa wito wa kutekelezwa kikamilifu usitishaji wa vita na anawaombea amani wananchi wa Palestina.
Rais Nangolo Mbumba wa Namibia pia amepongeza makubaliano kati ya Hamas na Israel. Amesema anaunga mkono usitishaji vita wa kudumu uliotangazwa na serikali ya Qatar.
Amesema watu wa Gaza wamepitia kipindi kigumu na kuvumilia mateso makubwa tangu Oktoba 7 mwaka 2023 walipokabiliwa na ukatili wa kutisha uliopelekea kuuliwa makumi ya maelfu ya watu wasio na hatia, kusababisha uharibifu na maafa makubwa ya miundombinu na kukiukwa waziwazi sheria za kimataifa za kibinadamu.
Rais wa Namibia ameongeza kuwa makubaliano ya kuitisha vita yaliyofikiwa kati ya Israel na harakati ya Hamas ni fursa kwa watu wa Gaza na yatapelekea kurejea katika ardhi yao na kuanza mchakato wa ujenzi mpya.