Israel yavamia meli za Freedom Flotilla na kuwakamata washiriki 100
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i138460-israel_yavamia_meli_za_freedom_flotilla_na_kuwakamata_washiriki_100
Vyombo vya habari vimeripoti kwamba makomandoo wa jeshi la Wanamaji la Israel wamevamia msafara wa meli za misaada ya kibinadamu kwa ajili ya watu wa Ukanda wa Gaza "Global Sumud Flotilla," ambao ulianza safari Alhamisi iliyopita kutoka Uturuki kuelekea Ukanda wa Gaza.
(last modified 2026-05-19T04:02:24+00:00 )
May 19, 2026 04:00 UTC
  • Israel yavamia meli za Freedom Flotilla na kuwakamata washiriki 100

Vyombo vya habari vimeripoti kwamba makomandoo wa jeshi la Wanamaji la Israel wamevamia msafara wa meli za misaada ya kibinadamu kwa ajili ya watu wa Ukanda wa Gaza "Global Sumud Flotilla," ambao ulianza safari Alhamisi iliyopita kutoka Uturuki kuelekea Ukanda wa Gaza.

Uvamizi huo umefanyika mamia ya kilomita kutoka pwani ya Cyprus (Kupro).

Kituo cha Israel cha Channel 12 kimemnukuu afisa wa utawala huo akisema udhibiti wa meli za msafara huo umefanyika kwa kasi kubwa na kwamba mateka wamehamishiwa kwenye meli nyingine.

Waandaaji wa Freedom Flotilla wamesema katika taarifa yao kwamba jeshi la Israel limezuia msafara huo wa meli, na kwamba askari wa Israel wamevamia meli na boti za msafara huo mchana kweupe.

Waandaaji pia wametoa wito kwa serikali za nchi mbalimbali kuchukua hatua za kukomesha vitendo vya uharamia vinavyolenga kudumisha mzingiro wa Israel dhidi ya watu wa Ukanda wa Gaza.

Wakati huo huo Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) imelaani uvamizi wa Israel dhidi ya msafara huo wa misaada ya kibinadamu ikisema kwamba "shambulio la kigaidi la Israel kwenye msafara wa meli wa Freedom Flotilla ni kitendo kamili cha uharamia."

Hamas imetoa wito wa kuwawajibisha viongozi wa Israel kwa kukiuka sheria za kimataifa, kuwaachilia huru wanaharakati wa Freedom Flotilla, na kukomesha mzingiro haramu wa Gaza.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Uturuki pia imelaani shambulio hilo dhidi ya meli za msafara wa misaada ya kibinadamu kwa ajili ya Gaza katika maji ya kimataifa, ikilitaja kuwa ni kitendo kipya cha uharamia.