UN: Mapambano dhidi ya ugaidi barani Afrika yaheshimu haki za binadamu
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i121764-un_mapambano_dhidi_ya_ugaidi_barani_afrika_yaheshimu_haki_za_binadamu
Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema kuwa, mapambano ya kukabiliana kikamilifu na ugaidi barani Afrika yanapaswa kuhusisha uvumbuzi na mtazamo unaoheshimu haki za binadamu na utawala wa sheria.
(last modified 2025-01-22T13:33:03+00:00 )
Jan 22, 2025 13:33 UTC
  • Amina J. Mohammed
    Amina J. Mohammed

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema kuwa, mapambano ya kukabiliana kikamilifu na ugaidi barani Afrika yanapaswa kuhusisha uvumbuzi na mtazamo unaoheshimu haki za binadamu na utawala wa sheria.

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Amina J. Mohammed ameutaja ugaidi kuwa tishio kubwa zaidi kwa amani, usalama na maendeleo endelevu katika bara zima la Afrika, akisisitiza kuwa kupambana na chimbuko la ugaidi ukiwemo umaskini, ukosefu wa usawa na kukatishwa tamaa, kunapaswa kuwa kipaumbele barani Afrika. 

Vilevile ametilia mkazo suala la kuchukuliwa hatua zinazozingatia haki za binadamu na ushirikiano wa kikanda ili kuratibu hatua za kukabiliana na ugaidi barani Afrika.

Amina Mohammed amesema kuwa kutengwa vijana wa Kiafrika, pamoja na viwango vya juu vya ukosefu wa ajira, kumekiweka kizazi kizima katika hatari ya makundi yenye itikadi kali, na kuongeza kuwa: "Iwapo hatutachukua hatua, tutapoteza kizazi hiki kwa makundi ya kigaidi."

Amina J. Mohammed

Wakati huo huo, Bankole Adeoye, Kamishna wa Umoja wa Afrika wa Masuala ya Kisiasa, Amani na Usalama, pia amekiambia kikao cha Baraza la Usalama kwamba mwaka jana, Kituo cha Kupambana na Ugaidi cha Umoja wa Afrika (AUTUC) kilirekodi jumla ya mashambulizi 3,400 ya kigaidi katika bara hilo na kwamba mashambulizi haya yalisababisha vifo vya zaidi ya watu 13,900.

Kwa upande wake, Vassily Nebenzia, mwakilishi wa kudumu wa Russia katika Umoja wa Mataifa amesema: "Mahesabu potofu na vitendo vilivyo kinyume cha sheria vya nchi za Magharibi vimechangia pakubwa kuenea kwa ugaidi barani Afrika."