Mashindano ya Kimataifa ya Qur'ani Yafunguliwa Algeria
Mashindano ya 20 ya Kimataifa ya Kuhifadhi na Kusoma Qur'ani ya Algeria yamefunguliwa huko Algiers, mji mkuu wa Algeria.
Mashindano hayo yamefunguliwa katika Klabu ya Kitaifa ya Jeshi la Algeria yakihudhuriwa na Youcef Belmehdi, Waziri wa Masuala ya Kidini na Wakfu, Ibrahim Mourad, Waziri wa Mambo ya Ndani, na maafisa kadhaa wa serikali na wanadiplomasia wa kigeni nchini Algeria.
Waziri wa Masuala ya Dini na Wakfu wa Algeria amesema katika hotuba ya ufunguzi wa mashindano hayo kwamba: "Mashindano haya yanafanyika katika mwezi wa Rajab kwa ajili ya kuenzi tukio la safari ya Israa na Mi'raji ya Mtume Muhammad (SAW) sambamba na maadhimisho ya miaka 70 ya Mapinduzi ya Ukombozi wa Algeria."
Ameongeza kuwa: “Usimamizi wa Rais wa Algeria wa programu mbalimbali za kidini unadhihirisha jinsi anavyojali na kutilia mkazo suala la kueneza mafundisho ya Kiislamu na Qur’ani na kuhifadhi utambulisho wa kitaifa, na kufanyika Mashindano ya Kimataifa ya Qur’ani katika toleo lake la 20 baada ya miongo miwili ya mashindano haya ni kielelezo cha ukweli huo."

Youcef Belmehdi amesema: "Tangu miaka iliyopita, kinyang'anyoro hiki kimeshuhudia mashindano ya wahifadhi 900 wa Qur'ani na mahudhurio ya wasomi na maqari kutoka zaidi ya nchi 30 ili kusimamia kamati za majaji."
Kinyang'anyiro cha mashindano haya baina ya maqari kutoka nchi mbalimbali kinaanza leo Jumatano na kitaendelea hadi Jumamosi Februari 25. Hafla ya kufunga mashindano hayo ya Qur'ani itafanyika Jumapili ijayo, Januari 26, ambapo washindi watatu bora katika kila kipengele watatunukiwa zawadi zao.