Jeshi la Sudan: Tumevunja mzingiro wa RSF Khartoum
Jeshi la Sudan limetangaza habari ya kufanikiwa kuvunja 'mzingiro' uliowekwa na Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF) dhidi ya Kamandi Kuu ya jeshi hilo katikati mwa Khartoum, mji mkuu wa nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.
Taarifa ya jeshi hilo imesema kuwa, askari wake wamefanikiwa kuvunja mzingiro wa kambi yake ya Signal Corps, moja ya vituo vikubwa zaidi vya kijeshi katika mji huo, iliyoko Khartoum Bahri. Wanajeshi hao kisha walivuka Mto Nile ili kuungana na vikosi vya Khartoum ya Kati, ambayo pia ilikuwa imezingirwa.
Hata hivyo RSF imekanusha vikali madai hayo, ikisisitiza kuwa ripoti hizo ni propaganda ya jeshi la serikali inayolenga kuwapa moyo na ari wanajeshi wa serikali. Kikosi hicho kinadai kuwa jeshi la Sudan linaeneza habari hizo za uwongo na upotoshaji kupitia video bandia zilizotiwa mkono.
Kusonga mbele huko kama kutathibiti kutakuwa mafanikio makubwa kwa jeshi la Sudan katika mji mkuu, ambapo vikosi vya RSF vimekuwa na uwepo mkubwa na kuzingirwa Kamandi Kuu ya jeshi, kambi yake ya Signal Corps, na Ikulu ya Rais.
Wakati huo huo, watu wasiopungua wanane wameuawa huku makumi ya wengine wakijeruhiwa katika shambulizi la mizinga la RSF lililolenga kambi ya wakimbizi ya Abu Shouk magharibi mwa Sudan.

Kamati ya Dharura ya Abu Shouk, inayoundwa na wanaharakati na watu waliojitolea kutoa misaada, imetoa taarifa ikisema kwamba, wanamgambo wa RSF walishambulia vikali kambi ya El Fasher kwa mizinga mikubwa jana Ijumaa.
Mzozo kati ya jeshi la Sudan na Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF) ulioanza katikati ya Aprili 2023 umesababisha kuuawa watu zaidi ya 20,000 na milioni 14 kuwa wakimbizi. Ripoti hii ni kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa.