Museveni apuuza uamuzi wa mahakama juu ya mahakama za kijeshi
Rais wa Uganda, Yoweri Museveni amesema serikali yake itaendelea kuwashtaki raia katika mahakama za kijeshi, licha ya Mahakama ya Juu ya nchi hiyo kupiga marufuku hatua hiyo, ikisema ni kinyume cha katiba.
Ijumaa ya Januari 31, 2025, Mahakama ya Juu ya Uganda ilisema mahakama za kijeshi hazina mamlaka ya kuwahukumu raia, na kuamuru kesi zote zinazoendelea za kiraia katika mahakama za kijeshi kuhamishiwa kwenye mfumo wa mahakama ya kiraia ya nchi hiyo.
Uamuzi huo umepongezwa na wakili wa kiongozi mkuu wa upinzani Uganda, Kizza Besigye ambaye anakabiliwa na kesi katika mahakama kuu ya kijeshi nchini humo.
Katika taarifa kwa vyombo vya habari jana Jumamosi, Museveni amesema uamuzi wa Mahakama ya Juu sio sahihi na kueleza kuwa, mashtaka katika mahakama ya kijeshi yanaimarisha mahakama za kiraia, na yamesaidia katika kutuliza Karamoja, eneo la kaskazini mashariki mwa Uganda lililokumbwa na ghasia na mapigano kwa kutumia silaha.

"Nchi haiongozwi na majaji," Museveni amesema na kuongeza kwa kusema, "Mahakama ya kijeshi ilitusaidia kuitia adabu Karamoja. Katu hatutaachana na chombo hiki muhimu kwa ajili ya kudumisha utulivu."
Wanaharakati wa haki za binadamu kwa muda mrefu wamekuwa wakiishutumu serikali ya Museveni kwa kutumia mahakama za kijeshi kuwashitaki viongozi wa upinzani na wafuasi wao kwa tuhuma zilizochochewa kisiasa. Kwa miaka mingi, mahakama za kijeshi zimewahukumu mamia ya raia, wakiwemo wapinzani wa kisiasa na wakosoaji wa serikali.