Uganda yatuma askari 1,000 zaidi mashariki mwa DRC
(last modified Wed, 05 Feb 2025 02:40:58 GMT )
Feb 05, 2025 02:40 UTC
  • Uganda yatuma askari 1,000 zaidi mashariki mwa DRC

Uganda imeripotiwa kutuma wanajeshi zaidi ya 1,000 wa ziada huko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ndani ya wiki moja iliyopita, karibu na eneo ambalo wanajeshi wa serikali ya Kinshasa wanapambana na waasi wa M23.

Vyanzo vya Umoja wa Mataifa vimeripoti kuwa, hatua hiyo imeongeza idadi ya wanajeshi wa Uganda waliotumwa rasmi kuiunga mkono serikali ya Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Felix Tshisekedi, hadi karibu 5,000.

Duru za habari zimeiambia Reuters kuwa, Uganda imekuwa ikilisaidia jeshi la Kongo dhidi ya kundi jingine la waasi la ADF, na kutumwa wanajeshi zaidi ambao idadi yao ni kati ya 1,000 na 2,000, kumefanyika chini ya mwamvuli wa 'Operesheni Shujaa.'

Hata hivyo, Msemaji wa Jeshi la Uganda, Felix Kulayigye bila kutoa maelezo zaidi, amekanusha ripoti za kutumwa kwa kikosi kipya, akisema vikosi vya nchi hiyo vilivyokuwa DRC, vimebadilisha "mbinu yao ya ulinzi".

Wakati huo huo, Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini ameahidi kuendelea kuisaidia Kongo DR licha ya Waafrika Kusini kutoa wito wa kuondoka Kongo wanajeshi wa nchi hiyo kufuatia vifo vya walinda amani 14 wa Afrika Kusini.

Askari wa Uganda mashariki mwa DRC

Haya yanajiri huku muungano wa waasi wa 'The Alliance Fleuve Congo' mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo unaolijumuisha pia kundi la waasi wa M23, ukitangaza kusitisha mapigano kuanzia jana Jumanne.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani, zaidi ya watu 900 wameuawa katika wiki mbili zilizopita katika mji wa mashariki wa Goma wakati wa mapigano kati ya waasi wa M23 na vikosi vya serikali.