Shule zaendelea kuchomwa Kenya, wasiwasi watanda
Vitendo vya kuchoma moto shule vinavyoshadidi kila uchao huko Kenya vimeitia wasiwasi mkubwa serikali ya nchi hiyo.
Waziri wa Elimu wa Kenya, Fred Matiang'i ameeleza wasiwasi wake kuhusu matukio hayo ya kuchomwa shule nchini humo katika mazungumzo aliyofanya Ijumaa hii na wawakilishi wa walimu, viongozi wa dini na maafisa uchunguzi na kubadilishana nao mawazo kuhusu suala hilo.
Shule 130 zimechomwa moto Kenya katika miezi mitatu ya hivi karibuni, suala ambalo limesababisha hasara kubwa. Viongozi na wananchi wa Kenya wametoa maoni na mitazamo tofauti kuhusu malengo halisi ya vitendo hivyo viovu vya kuchomwa moto shule ambavyo vimekuwa mgogoro wa kitaifa.
Juzi usiku peke yake shule tano zilichomwa moto nchini Kenya. Wanafunzi karibu 150 na walimu 10 wamekwishatiwa nguvuni wakihusishwa na hujuma hiyo ya kuchoma moto shule.
Gazeti la Star linalochapishwa jijini Nairobi limemuomba Rais Uhuru Kenyatta achukue hatua haraka iwezekanavyo ili kukomesha uwendawazi huo wa kuchoma moto shule nchini Kenya.