Ivory Coast yatangaza tarehe ya kuondoka wanajeshi wa Ufaransa nchini humo
Serikali ya Ivory Coast imeainisha tarehe ya kuondoka wanajeshi 'vamizi' wa Ufaransa katika nchi hiyo ya Afrika Magharibi.
Vyanzo vya habari nchini Ufaransa na Ivory Coast vimeliambia shirika la habari la AFP kwamba, uondoaji wa wanajeshi wa Ufaransa umepangwa tarehe 20 Februari, na Kodivaa inasisitiza kuwa "iko tayari" kuondolewa kwa vikosi hivi.
Kwa mujibu wa Pars Today, ikinukuu IRNA, Ufaransa ina wanajeshi wapatao 1,000 nchini Ivory Coast, lakini kuna uwezekano kuwa askari 80 wa nchi hiyo ya Ulaya watasalia katika nchi hiyo ya Kiafrika kuendelea 'kutoa mafunzo' kwa vikosi vya Kodivaa.
Habari zaidi zinasema kuwa, kambi ya Kikosi cha 43 cha Wanamaji huko Port Bouet itarejeshwa kwa wanajeshi wa Ivory Coast baada ya kuondoka wanajeshi wa Ufaransa.
Hapo awali, Rais Alassane Ouattara wa Ivory Coast alisema kuwa wanajeshi wa Ufaransa wangeondoka nchini humo mwezi uliopita wa Januari. Rais wa Ivory Coast alieleza haya katika hotuba yake ya mwisho wa mwaka kwa taifa.
Hatua hii ya Ivory Coast inafuatia uamuzi sawa uliochukuliwa na serikali za Mali, Burkina Faso na Niger. Aidha serikali ya Chad ilitangaza tarehe 28 Novemba mwaka jana kwamba, imefuta makubaliano yake ya kijeshi na serikali ya Ufaransa kuhusu uwepo wa wanajeshi 1,000 wa Ufaransa nchini humo.
Ufaransa ilikoloni nchi 20 za Kiafrika kwa miongo kadhaa. Baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia na wimbi la mapambano ya uhuru dhidi ya wakoloni wa Ulaya katika nchi za Afrika, Ufaransa ilijaribu kudumisha ushawishi wake barani Afrika na uwepo wa kijeshi katika baadhi ya makoloni yake ya zamani.