Mzozo wa DRC: Bunge la Rwanda lalaani azimio la EU dhidi yake
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i123066
Bunge la Rwanda limekosoa vikali azimio lililopasishwa hivi karibuni na Bunge la Ulaya, likidai kuwa Rwanda linahusika na mzozo na machafuko yanayoendelea mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
(last modified 2025-02-22T11:58:51+00:00 )
Feb 22, 2025 11:58 UTC
  • Mzozo wa DRC: Bunge la Rwanda lalaani azimio la EU dhidi yake

Bunge la Rwanda limekosoa vikali azimio lililopasishwa hivi karibuni na Bunge la Ulaya, likidai kuwa Rwanda linahusika na mzozo na machafuko yanayoendelea mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Katika kikao chao cha jana, Wabunge wa Rwanda walipasisha azimio walizitaka nchi zote, za kieneo na taasisi za kimataifa kujizuia kupasisha na kueneza taarifa za upande mmoja, kama lilivyofanya Bunge la Ulaya.

Bunge la Rwanda (ikiwemo Seneti na Baraza la Manaibu), limesisitiza kuwa, badala ya Bunge la Umoja wa Ulaya kuilaumu serikali ya Kigali, linapasa kuzihimiza pande husika kwenye mgogoro wa DRC kufanya mazungumzo ya maana, ambayo yataleta amani ya kudumu katika eneo pana la Maziwa Makuu.

Bunge la EU katika kikao cha karibuni, mbali kutishia kuiwekea Rwanda msururu wa vikwazo vikiwemo vya kiuchumi, liliitaka serikali ya Kigali kuviondoa eti 'vikosi vyake' mashariki ya DRC. 

Hiyo jana pia, serikali ya Kigali ililaani vikali hatua ya Wizara ya Hazina (Fedha) ya Marekani ya kumwekea vikwazo Waziri wa Utangamano wa Kieneo wa Rwanda, Jenerali (Mstaafu) James Kabarebe, kwa tuhuma za kuhusika na mzozo na machafuko yanayoendelea mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

M23; Rwanda inakanusha kuliunga mkono kundi hilo la waasi mashariki DRC

Katika hatua nyingine, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa jana Ijumaa lilitoa wito kwa jeshi la Rwanda kuacha kuunga mkono kundi la waasi la M23 mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, na kuwaondoa mara moja wanajeshi wote katika eneo la Kongo "bila masharti."

Baraza hilo lenye wajumbe 15 kwa kauli moja lilipitisha azimio lililoandaliwa na Ufaransa na kuzitaka DRC na Rwanda kurejea katika mazungumzo ya kidiplomasia ili kufikia azimio la kudumu la amani.