Misri yapinga pendekezo la Israel la kutaka Gaza isimamiwe na Cairo
(last modified Thu, 27 Feb 2025 11:01:40 GMT )
Feb 27, 2025 11:01 UTC
  • Misri yapinga pendekezo la Israel la kutaka Gaza isimamiwe na Cairo

Misri imepinga pendekezo lililotolewa na kiongozi wa upinzani wa Israel, Yair Lapid kwamba Cairo, badala ya Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina Hamas, iendeshe na kuusimamia kwa muda Ukanda wa Gaza; na kusisitiza kuwa mipango ya aina hiyo "haikubaliki."

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Misri, Tamim Khalaf amenukuliwa na shirika la habari la serikali MENA akisema kuwa, "Dhana au mapendekezo yoyote ambayo yanakiuka msimamo wa Misri na Waarabu (kuhusu Gaza)... yanakataliwa na hayakubaliki."

Khalaf amekariri wito wa Misri wa kutaka kuondoka Israel katika ardhi ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu, na uungaji mkono wake wa kuanzishwa "taifa huru la Palestina."

Ameashiria "maingiliano ya asili" kati ya Gaza, Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu na al-Quds Mashariki na kusema kuwa maeneo hayo yanawakilisha "eneo la taifa huru la Palestina na lazima liwe chini ya mamlaka na utawala kamili wa Palestina."

Siku ya Jumanne, Yair Lapid, kiongozi wa upinzani wa Israel alizindua kile alichokiita 'mpango wa Gaza' eti baada ya vita kumalizika. Chini ya mpango wake huo, Misri inapasa kuchukua udhibiti wa ukanda huo mara tu utekeleza wa sasa wa makubaliano ya kusitisha mapigano utakapokamilika, mkabala wa msamaha mkubwa wa madeni.

Magofu Gaza yaliyosababishwa na mabomu ya Wazayuni

"Suluhu ni kwamba Misri itachukua jukumu la usimamizi wa Ukanda wa Gaza kwa miaka minane, na chaguo la kuongeza hadi miaka 15," Lapid aliiambia taasisi ya kushupalia vita ya Foundation for Defense of Democracies (FDD) huko Washington.

Pendekezo la Lapid limekuja baada ya mpango tata wa Rais wa Marekani, Donald Trump wa "kutwaa" Gaza na kuwahamisha Wapalestina kutoka ukanda huo na kuwapeleka katika nchi jirani kukataliwa si tu na Misri, bali na jamii ya kimataifa.