Misri yapinga kuundwa serikali nyingine nchini Sudan
(last modified Sun, 02 Mar 2025 12:24:07 GMT )
Mar 02, 2025 12:24 UTC
  • Misri yapinga kuundwa serikali nyingine nchini Sudan

Misri imetangaza leo Jumapili kuwa haiafiki jaribio lolote la kuunda serikali nyingine nchini Sudan au kuchukuliwa hatua yoyote ambayo inatishia umoja na mamlaka ya kujitawala Sudan.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Misri imesema katika taarifa kwamba: Jamhuri ya Kiarabu ya Misri inapinga majaribio yoyote ambayo yanatishia umoja, mamlaka ya kujitawala, na uhuru wa ardhi ya Sudan, ikiwa ni pamoja na juhudi za kuanzisha serikali nyingine nchini humo."

Imetahadharisha kwamba, majaribio kama hayo "yanafanya hali nchini Sudan kuwa mbaya zaidi, yanazuia juhudi zinazoendelea za kuleta pamoja maono ya mirengo ya kisiasa ya Sudan, na kuzidisha mzozo wa kibinadamu nchini humo."

Kadhalika Misri imezitaka pande zote za Sudan "kutanguliza mbele maslahi ya kitaifa ya nchi na kushiriki vyema katika kuanzisha mchakato jumuishi wa kisiasa bila uingiliaji wa nje."

Mnamo Februari 22, kundi la wanamgambo wa Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF), pamoja na makundi ya kisiasa ya Sudan na makundi yenye silaha, walitia saini mkataba wa kisiasa mjini Nairobi, Kenya, kwa shabaha ya kuunda serikali nyingine inayopinga mamlaka za Sudan.

Wanamgambo wa RSF

Serikali ya Sudan hivi karibuni iliapa kuchukua hatua kali dhidi ya Kenya kutokana na hatua ya Nairobi kuwa mwenyeji wa kikao hicho cha wanamgambo wa RSF.

Hata hivyo Kenya ilitetea uamuzi wake huo, ikisema kuwa kuandaa mikutano hiyo ni sehemu ya juhudi zake za kutafuta suluhu za kumaliza vita nchini Sudan kwa uratibu wa Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika.