Kwa nini Rwanda imeitaka Uingereza iilipe fidia?
(last modified Fri, 07 Mar 2025 10:34:52 GMT )
Mar 07, 2025 10:34 UTC
  • Kwa nini Rwanda imeitaka Uingereza iilipe fidia?

Suala la madai ya Rwanda ya fidia ya pauni milioni 50 kutoka kwa Uingereza kwa kuacha mpango wa kuwafukuza wakimbizi haramu nchini humo sasa limekuwa kadhia tata na ngumu kati ya nchi hizo mbili.

Gazeti la Daily Mail, limeashiria makubaliano yaliyofikiwa baina ya Kigali na London ya kuwapatia makazi wahamiaji haramu nchini Rwanda, ambayo yaliibua upinzani mkubwa wa watetezi wengi wa haki za binadamu, na kuandika: Baada ya serikali ya Uingereza kufuta mpango wa kuwapa makazi wahamiaji haramu nchini Rwanda, nchi hiyo ya Afrika Mashariki sasa inataka kulipwa fidia ya pauni milioni 50. 

Mwaka jana, Uingereza na Rwanda zilitia saini mkataba wa miaka mitano ambapo kwa mujibu wake, Uingereza itatuma sehemu ya wahamiaji haramu nchini Rwanda na kuipa nchi hiyo msaada wa kifedha. Gharama ya awali ya mkataba huo ilikadiriwa kuwa zaidi ya pauni milioni 300, lakini kiutendaji, ni ndege moja tu iliyopeleka wahamiaji hao huko Rwanda, na mkataba huo umetelekezwa kutokana na upinzani mkali wa vyama vya siasa na mashirika ya kutetea haki za binadamu. Mkataba huo uliwekwa kando kivitendo mwezi Julai mwaka jana na Waziri Mkuu wa Uingereza, Keir Starmer.

Keir Starmer

Suala la kupeleka wahamiaji haramu kutoka mataifa ya Ulaya kwenda barani Afrika na kuwapa makazi katika baadhi ya nchi za bara hilo limekuwa katika ajenda za nchi za Ulaya katika miaka michache iliyopita, kama suluhisho la kukabiliana na wimbi la uhamiaji haramu kuelekea barani Ulaya. Katika mkondo huo, nchi za Ulaya zimetia saini mikataba na baadhi ya nchi za Kiafrika, kama Rwanda, na kwa kutumia ahadi ya kitita cha fedha na msaada wa kiuchumi, zimejaribu kuwapa makazi wahamiaji walioingia Ulaya katika za Kiafrika. Hata hivyo, hali ngumu katika makazi ya wakimbizi hao, ukosefu wa vifaa vya kutosha, na kutokuwepo sheria zinazofaa na za uwazi katika suala hili vimeifanya sera hii ikose ufanisi kwa nchi za Ulaya.

Hii ni pamoja na kuwa, mchakato usiofaa wa utekelezaji wa maamuzi hayo umeibua hasira za vyama vingi na watetezi wa haki za binadamu duniani kote. Lakini kwa upande mwingine, baadhi ya nchi za Afrika zimekuwa tayari kukubali mpango huo kutokana na mahitaji ya kifedha na kutaka himaya na uungaji mkono wa kisiasa wa nchi za Magharibi.

Tunaweza kusema kuwa, katika miaka ya hivi karibuni, baadhi ya nchi za Kiafrika zimekaribisha mapendekezo ya nchi za Ulaya ya kuwapokea wahamiaji kwa sababu mbalimbali, kama vile haja ya kupata misaada ya kifedha na kiuchumi, kuvutia uungaji mkono wa nchi za Magharibi kwa ajili ya kutekeleza miradi ya miundombinu ya kiuchumi na kijamii, na kupata misaada ya Ulaya kwa ajili ya kukabiliana na makundi ya kigaidi na ukosefu wa usalama. Kwa maana kwamba, baadhi ya nchi hizo za Afrika, zimekubali sera za Ulaya ili kuboresha uhusiano wao na nchi za bara hilo na kwa njia fulani, kupanua uhusiano wao wa kigeni. Nyingi kati ya nchi hizo ambazo zinakabiliwa na matatizo makubwa ya kiuchumi, harakati za makundi ya kigaidi na ukosefu wa usalama wa kisiasa na kijamii, zinayaona mapendekezo hayo kuwa ni fursa na zinakhitari kuyakubali kwa nia ya kubadilisha hali hiyo kwa manufaa yao.

Lakini katika hali halisi, mikataba hiyo haijatekelezwa, na nchi za Ulaya hazijatoa hata msaada wa kisiasa kwa nchi husika za Kiafrika. Mfano wa wazi wa ukweli huo ni mvutano unaoonekana sasa baina ya Kigali na London. Sasa, kufuatia mgogoro na vita nchini Kongo, Lord Collins, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza, ameishutumu Rwanda kuwa inawaunga mkono waasi nchini Kongo na kuingilia masuala ya ndani na vita vya nchi hiyo.