Jeshi: Watu 10 wauawa, 23 wajeruhiwa katika shambulio la RSF Sudan
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i123858-jeshi_watu_10_wauawa_23_wajeruhiwa_katika_shambulio_la_rsf_sudan
Jeshi la Sudan (SAF) limetangaza kuwa, takriban watu 10 wameuawa na wengine 23 kujeruhiwa katika mashambulizi ya makombora yaliyofanywa na Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) kwenye vitongoji vya makazi ya watu huko El Fasher, makao makuu ya Jimbo la Darfur Kaskazini la magharibi mwa Sudan.
(last modified 2025-03-13T06:25:48+00:00 )
Mar 13, 2025 06:25 UTC
  • Jeshi: Watu 10 wauawa, 23 wajeruhiwa katika shambulio la RSF Sudan

Jeshi la Sudan (SAF) limetangaza kuwa, takriban watu 10 wameuawa na wengine 23 kujeruhiwa katika mashambulizi ya makombora yaliyofanywa na Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) kwenye vitongoji vya makazi ya watu huko El Fasher, makao makuu ya Jimbo la Darfur Kaskazini la magharibi mwa Sudan.

Taarifa ya Jeshi la Sudan imesema: "Katika uhalifu wao mpya dhidi ya raia, wanamgambo waasi wameshambulia vitongoji vya raia katika mji wa El Fasher."

Taarifa hiyo pia imesema: "Shambulio hili limesababisha vifo vya watu 10, akiwemo msichana mmoja wa miaka 3, na kuwaacha wengine 23 wakiwa na majeraha, baadhi yao wamepata majeraha mabaya na wamepelekwa haraka kwenye vituo vya matibabu."

Taarifa ya jeshi la Sudan imeendelea kusema: "Waasi wa RSF wameanza kutumia droni na ndege zisizo na rubani kulenga maeneo muhimu ndani ya mji El Fasher, lakini kikosi cha ulinzi wa anga vya jeshi kimefanikiwa kutungua droni hizo.

Vikosi vya Ulinzi wa Harakati RSF havikuwa vimetoa taarifa yoyote kuhusu madai hayo ya kufanya mashambulizi kwenye mji wa El Fasher. Mji huo umekuwa ni uwanja wa mapigano makali kati ya SAF na RSF tangu Mei 10 mwaka jana.

Sudan imetumbukia kwenye mgogoro mbaya wa uchu wa madaraka baina ya majenerali wa kijeshi wanaoongoza makundi mawili ya SAF na RSF tangu katikati ya mwezi Aprili 2023. Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, hadi hivi sasa mapigano hayo yameshaua watu 29,683. 

Kwa upande wake, Shirika la Kimataifa la Uhamiaji limesema kuwa, mgogoro wa Sudan umewakosesha makazi zaidi ya watu milioni 15 ndani na nje ya nchi hiyo.