IGAD yatakiwa kuishawishi Sudan Kusini kuwachilia huru wapinzani
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i123860-igad_yatakiwa_kuishawishi_sudan_kusini_kuwachilia_huru_wapinzani
Chama kikuu cha upinzani huko Sudan Kusini, cha Sudan People's Liberation Movement/Army-In Opposition (SPLM/A-IO) kinachoongozwa na Makamu wa Kwanza wa Rais, Riek Machar, kimezihimiza Jumuiya ya IGAD na Jumuiya ya Afrika Mashariki EAC kuingilia kati na kusaidia kuachiliwa huru maafisa kadhaa wa upinzani wanaoshikiliwa na serikai ya Sudan Kusini.
(last modified 2025-03-13T06:27:26+00:00 )
Mar 13, 2025 06:27 UTC
  • IGAD yatakiwa kuishawishi Sudan Kusini kuwachilia huru wapinzani

Chama kikuu cha upinzani huko Sudan Kusini, cha Sudan People's Liberation Movement/Army-In Opposition (SPLM/A-IO) kinachoongozwa na Makamu wa Kwanza wa Rais, Riek Machar, kimezihimiza Jumuiya ya IGAD na Jumuiya ya Afrika Mashariki EAC kuingilia kati na kusaidia kuachiliwa huru maafisa kadhaa wa upinzani wanaoshikiliwa na serikai ya Sudan Kusini.

Pal Mai Deng, waziri wa rasilimali za maji na umwagiliaji ambaye pia ni msemaji wa SPLM/A-IO, amesema kuwa, nchi wanachama wa IGAD zina wajibu wa kushiriki na kuwezesha utatuzi wa amani kwa mgogoro unaoendelea.

Katika taarifa yake aliyoitoa huko Juba, mji mkuu wa Sudan Kusini, Deng pia amesema: "Aidha tunatoa mwito kwa nchi wanachama wa IGAD kuingilia kati na kusaidia kuachiliwa huru viongozi wa kisiasa na kijeshi wa SPLM/A-IO."

Mvutano kati ya serikali ya mpito ya Sudan Kusini na upinzani umechochewa na mapigano ya Machi 3 kati ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Sudan Kusini na Jeshi la White, ambalo linahusishwa na SPLM/A-IO, kwenye eneo la Nasir la Jimbo la Upper Nile.

Wiki iliyopita, zaidi ya dazeni mbili za wanajeshi wa Sudan Kusini, akiwemo jenerali mmoja, waliuawa wakati helikopta ya ujumbe wa Umoja wa Mataifa ilipotunguliwa kwa kombora huko Nasir.

Katikati ya mvutano huo unaozidi kuongezeka, serikali ya Sudan Kusini imeamua kuwakamata na kuwaweka chini ya ulinzi maafisa wakuu wa kijeshi na mawaziri watiifu kwa SPLM/A-IO.

Chama cha Sudan People's Liberation Movement kinachoongozwa na Rais Salva Kiir Mayardit kilitiliana saini makubaliano ya amani na chama cha SPLM/A-IO; mwaka 2018 kwa shabaha ya kumaliza mgogoro wa miaka mingi baina ya makundi hayo hasimu.