Sudan Yapiga marufuku bidhaa za Kenya kwa kusaidia waasi wa RSF
Sudan imetangaza kuwa inasitisha uagizaji wa bidhaa zote kutoka Kenya kutokana na hatua ya Kenya kukubali kufanyika nchini humo mikutano ya kundi la waasi linalojulikana kama Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) na washirika wake.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Sudan (SUNA), amri hiyo ilitolewa na Waziri wa Biashara na Ugavi wa Sudan, Omar Ahmed Mohamed Ali.
Taarifa ya wizara ilieleza kuwa marufuku hiyo iliyoanza Alhamisi ni hatua ya kulinda maslahi ya kitaifa na usalama wa Sudan, kutokana na kile ilichokiita mwenendo wa Kenya wa kusaidia na kufadhili shughuli za waasi wa RSF.
Hadi sasa, serikali ya Kenya haijatoa majibu rasmi kufuatia uamuzi huo. Sudan huagiza idadi kubwa ya bidhaa kadhaa kutoka Kenya, ikiwemo chai, chakula, na dawa.
Hatua hii inafuatia mkataba wa kisiasa ulio sainiwa Februari 22 nchini Kenya kati ya RSF na makundi ya kisiasa na kijeshi ya Sudan kwa lengo la kuunda serikali inayopinga mamlaka ya Sudan.
Serikali ya Sudan ilipinga vikali uenyeji wa Kenya wa kile ilichokiita ‘njama ya RSF kuanzisha serikali ’. Mnamo Februari 20, Sudan ilimuita balozi wake nchini Kenya, Kamal Jabara, kama ishara ya kupinga ushiriki wa Kenya katika mazungumzo hayo.
Hata hivyo, Kenya ilitetea hatua yake, ikisema kuwa kuandaa mikutano hiyo ni sehemu ya juhudi za kutafuta suluhisho la kumaliza vita nchini Sudan, kwa kushirikiana na Umoja wa Mataifa (UN) na Umoja wa Afrika (AU).
Tangu Aprili 2023, jeshi la Sudan na waasi wa RSF wamekuwa wakipigana katika vita ambavyo vimepelekea zaidi ya watu 20,000 kuuawa na kuwafanya watu milioni 15 kuwa wakimbizi, kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa na mamlaka za ndani.
Takwimu kutoka Observatory of Economic Complexity (OEC) zinaonyesha kuwa Kenya iliuza bidhaa zenye thamani ya dola milioni 48.2 kwa Sudan mnamo 2023. Bidhaa kuu zilizouzwa ni chai (dola milioni 29.6).
Mauzo ya Kenya kwa Sudan yamepungua kwa kiwango cha wastani cha 7.07% kila mwaka katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, yakishuka kutoka dola milioni 69.5 mwaka 2018 hadi dola milioni 48.2 mwaka 2023.