AU yatahadharisha kuhusu hali mbaya katika eneo la Tigray nchini Ethiopia
Umoja wa Afrika (AU) umeelezea wasiwasi wake mkubwa kuhusu matukio yanayojiri katika eneo la Tigray nchini Ethiopia, ambapo mizozo ya kisiasa kati ya pande zinazohasimiana inatishia makubaliano tete ya amani yaliyomaliza vita katika eneo hilo.
Katika taarifa rasmi iliyotolewa leo Ijumaa, Umoja Afrika umethibitisha kwamba unafuatilia kwa karibu mivutano inayoongezeka ndani ya chama cha Tigray People's Liberation Front, ukionya juu ya hatari ya hali ya sasa kwa amani na usalama wa kikanda.
Taarifa ya AU pia imesisitiza umuhimu wa kuheshimu makubaliano ya amani, ikitoa wito kwa pande zote kujizuia na kushiriki katika mazungumzo yenye kujenga ili kuepusha eneo hilo kutumbukia katika duru mpya ya ghasia na machafuko.
Umoja wa Afrika umethibitisha katika taarifa yake kwamba, kuna uudharura wa kuheshimiwa makubaliano ya amani ili kudumisha utulivu uliopatikana baada ya mateso ya muda mrefu na kuweka mazingira yanayofaa kwa maridhiano ya kitaifa na maendeleo endelevu katika eneo hilo.
Umoja wa Afrika pia umesisitiza umuhimu wa kupatikana suluhisho la kina la kisiasa ambalo linahakikisha ushiriki wa pande zote, ukionya kwamba kurudi nyuma kunaweza kuvuruga hali ya kibinadamu na kisiasa katika eneo hilo.
Kwa upande wake, Gavana wa Tigray ameonya kuwa eneo hilo linakabiliwa na mzozo mbaya wa kibinadamu kutokana na kuvurugwa juhudi za kuwarudisha watu waliokimbia makazi yao na migogoro ya ndani ambayo inayumbisha utulivu.
Gavana wa Tigray pia amelaani uwepo wa vikosi vya jeshi la Eritrea ndani ya eneo hilo, akiutaja kuwa ni tishio kubwa kwa amani. Vilevile ameitaka Serikali ya Shirikisho ya Ethiopia kutekeleza majukumu yake na kulinda eneo hilo dhidi ya uingiliaji wowote wa nje ambao unaweza kuzidisha hali mbaya.