Afrika Kusini: Tumesikitishwa na hatua ya Washington ya kumfukuza balozi wetu
-
Rais Cyril Ramaphosa
Afrika Kusini imetangaza kuwa uamuzi wa Marekani kumfukuza nchini humo balozi wake, Ebrahim Rasool "unasikitisha", lakini nchi hiyo "bado ina nia ya kujenga uhusiano wa kunufaishana" na Washington.
"Ofisi ya Rais imepokea hatua ya kusikitisha ya kufukuzwa Balozi wa Afrika Kusini nchini Marekani, Bw. Ebrahim Rasool," imesema taarifa iliyotolewa na Pretoria, ambayo imesisitiza kuwa "imedhamiria kujenga uhusiano wa kunufaisha" na Washington.
Ofisi ya Rais wa Afrika Kusini imewataka "washikadau wote wanaohusika na walioathiriwa kudumisha hali ya kidiplomasia katika ushirikiano wao na suala hilo" katika taarifa iliyotolewa mapema leo Jumamosi.
Taarifa hiyo imetolewa saa chache baada ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio kumtaja balozi wa Afrika Kusini nchini Marekani kuwa "hatakiwi" nchini humo, akisema "anachochea mivutano ya mbari", maneno ambayo yametajwa na Ofisi ya Rais wa Afrika Kusini kuwa ni "ya kusikitisha".
Haya yanajiri baada ya Rasool kushiriki katika mkutano wa taasisi ya wanafikra wa Afrika Kusini ambapo alisema kuwa kampeni ya Trump ya 'Make America Great Again' (Kuifanya Marekani Bora Tena), pamoja na ushawishi wa Elon Musk na Makamu wa Rais J.D. Vance, ni sehemu ya mtindo wa kimataifa wa kuhudumia wasiwasi (maslahi) ya Wazungu.
Aidha alisema kuwa Trump alitumia "silika ya upendeleo" na "ubaguzi wa rangi" kama "filimbi ya mbwa" wakati wa uchaguzi wa 2024.
Matamshi ya Rubio yanaashiria kuzorota zaidi kwa mahusiano ya Marekani na Afrika Kusini, ambayo tayari yaliingia doa kutokana na msimamo wa Pretoria wa kutetea haki za Wapalestina na kuifungua Israel mashtaka katika mahakama za kimataifa kwa tuhuma za kufanya mauaji ya kimbari dhidi ya raia wa Ukanda wa Gaza.
Hivi karibuni, Naibu Katibu Mkuu wa Kwanza wa chama tawala cha Afrika Kusini, ANC, Nomvula Mokonyane, akizungumza pambizoni mwa mkutano wa chama hicho uliofanyika Free State, aliunga mkono kauli ya Rais Cyril Ramaphosa kwamba Afrika Kusini haitakubali kutishwa na Marekani.