Raila: Nilizuia mapinduzi ya kijeshi dhidi ya Rais Ruto
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i123996-raila_nilizuia_mapinduzi_ya_kijeshi_dhidi_ya_rais_ruto
Kinara wa Upinzani Raila Odinga amefichua kuwa aliamua kumwokoa Rais William Ruto wakati wa maandamano ya Gen Z ili kuzima mapinduzi ya kijeshi ambayo yalikuwa yamesukwa na yalikuwa yakikaribia tu kutekelezwa.
(last modified 2025-03-16T09:08:02+00:00 )
Mar 16, 2025 09:08 UTC
  • Raila: Nilizuia mapinduzi ya kijeshi dhidi ya Rais Ruto

Kinara wa Upinzani Raila Odinga amefichua kuwa aliamua kumwokoa Rais William Ruto wakati wa maandamano ya Gen Z ili kuzima mapinduzi ya kijeshi ambayo yalikuwa yamesukwa na yalikuwa yakikaribia tu kutekelezwa.

Bw Odinga amekuwa akikosolewa na vijana nchini kuwa aliteka nyara wimbi lao la mageuzi, akalisambaratisha kisha akaungana na utawala wa Kenya Kwanza uliokuwa ukiwanyanyasa.

Waziri huyo Mkuu wa zamani alifunguka na kusema alipigiwa simu na ‘rafiki’ ambaye alimwomba aingilie kati kwa sababu jeshi lilikuwa likielekea kuung’oa utawala wa Rais Ruto iwapo maandamano yangeendelea kushtadi.

Waziri huyo Mkuu alisema kuwa baada ya Bunge la Kitaifa kuvamiwa mnamo Juni 25, na vijana kuanza maasi yao kwa kulenga Ikulu, ilikuwa dhahiri kwamba utawala wa Kenya Kwanza ulikuwa ukielekea kuporomoka.

Hali hiyo ililazimu Rais kuagiza majeshi yatoke kwenye makao yao ili yahakikishe  utulivu na amani vinakuwepo nchini baada ya polisi kulemewa na vijana.

“Ruto anaweza kuondolewa tu kupitia uchaguzi mkuu lakini unajua wanajeshi wakitoka kwenye kambi yao huwa hawarejei,” alisema Bw Odinga wakati wa mahojiano hayo.

Kiongozi huyo alifananisha hali ambayo Kenya ilijipata na yaliyotokea Misri wakati  kundi la Muslim Brotherhood (Ikhwanul Muslimin) lilipomwondoa mamlakani Rais Hosni Mubarak.

Kiongozi huyo wa upinzani alisimulia jinsi alivyotumia ushawishi wake wa kisiasa kuhakikisha Rais anatupilia mbali Mswada wa Fedha 2024 ambao ulikuwa unapingwa na vijana nchini.

Kuhusu ushirikiano wa sasa na serikali, Bw Odinga ameutaja kuwa bora zaidi na mkataba walioutia saini na Rais unalenga kukabili changamoto mbalimbali ambazo zimekuwa zikizonga Kenya.